Na Magreth Kinabo- Mahakama
Majaji
watatu wa Mahakama Kuu ya Tanzania leo tarehe 4 Mei, 2023
wameaagwa kitaaluma baada ya kustaafu utumishi wa Umma kwa kujibu wa sheria,
huku wakisisitiza watumishi wa Mahakama kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano,
weledi, uadilifu na upendo ili kuweza kutekeleza jukumu la utoaji haki na
kulinda uhuru wa Mahakama.
Majaji hao ambao wamestaafu
waliotoa kauli hizo kwa nyakati tofauti ni Mhe. Beatrice Mutungi, Mhe. John
Mgeta na Mhe. Sekela Moshi. Kwa pamoja wameishukuru Mahakama kwa ushirikiano
walioupata katika utumishi wao na kuiacha Mahakama katika mikono salama.
Aidha, Majaji hao waliasa
kwamba jukumu la utoaji haki linahitaji
uvumilifu na muda wa kujitolea kwa kiwango cha juu.
Kwa upande wake, Jaji Mutungi,
ambaye amekuwa mtumishi kwa Mahakama kwa miaka 33 amehudumu katika ngazi
mbalimbali, ikiwemo Hakimu Mkazi, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika
Kanda tofauti, zikiwemo Songea, Moshi na Dar es Salaaam.
Alisema mbali na kufanya
kazi kwa kuzingatia mambo mbalimbali, uwezo wa kutoa hukumu na maamuzi
mbalimbali umechangiwa na kuwa chini ya viongozi waelekezi na kupata mafunzo ya
kitaaluma ndani na nje ya nchi.
“Haki isitendeke tu bali
ionekane wazi na bila shaka inatendeka. Maana ya msemo huu ilinipasa kusikiliza
kwa umakini ushahidi wote ulioletwa na pande zote katika mashauri, kusoma na
kufanya utafiti ili niweze kufikia maamuzi yasiyokuwa na upendeleo. Rai yangu
kulingana na ukuaji wa sayansi na teknolojia mambo mengi yanabadilika. Hapa
nalenga kuwaasa kuwa Mahakama Mtandao ipewe kipaumbele,” alisema na kusisitiza watumishi
kupatiwa semina na mafunzo.
Akimzungumzia Jaji Mutungi,
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Moshi, Mhe. Dkt. Juliana Masabo alisema
anastahili kuigwa kwa uongozi wake mahiri, kuimarisha maadili ya watumishi na kuwasaidia
watumishi na wadau katika kutatua malalamiko.
Kwa upande wake, Jaji Moshi
ambaye amehudumu katika Mahakama kwa muda wa miaka 33 aliwasisitiza Mawakili wa
Serikali na wale wa kujtegemea kuzingatia
shajara zao ili kuepusha mashauri mengi kwa wakati mmoja. Kadhalika,
aliwaasa Mahakimu na Majaji kufanya ukaguzi katika masjala za Mahakama. Aliongeza
kuwa kazi ya ujaji ni ngumu inahitaji muda wa ziada ya saa za kazi.
Jaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Masajala Kuu, Mhe. Leila Mgonya, akimzungumzia Jaji Moshi alisema
atakumbukwa kwa uongozi mahiri na mwepesi wa kuchukua hatua, usimamizi wa
rasilimali watu, maono na ubunifu.
Naye Jaji Mgetta ambaye amehudumu
katika Mahakama kwa kipindi cha miaka 32 ameshika nafasi mbalimbali kutoka
Hakimu Mkazi na kuendelea kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu.
Alipata kozi mbalimbali fupi ndani na nje ya nchi ambazo zilimsaidia kupata
uzoefu, ikiwemo kuongeza thamani katika kazi yake.
“Ni muhimu kuzingatia
utawala wa sheria na wakati huo huo unasimamia haki za wananchi kwa mantiki
hiyo kunahitajika uharaka katika kutoa maamuzi na umakini wa ziada katika
maudhui ya maamuzi hayo kwa kuhakikisha yanakuwa sahihi,” alisema.
Jaji Mgetta alisema
mabadiliko ya sayansi na teknolojia yatumike vizuri ili kuhakikisha muda wa
kusikiliza mashauri unapungua na imani ya wananchi juu ya Mahakama inaongezeka.
Akimzunguzia Jaji Mgetta,
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Moses Mzuna alisena ni jasiri, alilinda
taswira ya taaluma, mwanadiplomasia, mkweli, myenyenyekevu na mwenye bidii,
Mwakilishi wa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, ambaye ni Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Mark Mulambo alisema Majaji
hao wana mchango mkubwa katika tasnia ya sheria kutokana na maamuzi
waliyoyatoa.
Makamu wa Rais wa Chama
cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Gloria Kalabamu aliwapongeza Majaji hao na
kuahidi kuwa TLS itaendelea kushiriana nao katika kupata ushauri, usaidizi katika tafiti na uzoefu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni