Na Arapha Rusheke, Mahakama Kuu Dodoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu hivi karibuni aliwaongoza watumishi wa Mahakama hiyo kumuaga Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kanda hiyo, Mhe. George Masaju ambaye ameteuliwa kuwa mshauri wa Rais kwenye masuala ya kisheria.
Hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi
wa Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kuhudhuriwa na
Majaji wa Mahakama Kuu kwenye Kanda hiyo, Mhe. Dkt. Adam Mambi, Mhe. Fatma
Khalfan na Mhe. Suleiman Hassan.
Alkizungumza katika hafla hiyo, Jaji
Mfawidhi alimweleza Mhe. Masaju
kuwa Serikali inatambua umuhimu wake na kazi zake alizofanya zimekuwa chachu ya
maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika katika Mahakama ya Tanzania.
“Serikali inatambua umuhimu na mchango wako katika kuimarisha maboresho
ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi katika Mahakama ya Tanzania, tutaendelea kuyafanyia
kazi yote ambayo umetushauri,” alisema Jaji Mdemu.
Kwa upande wake, Jaji Masaju ameushukuru uongozi wa Mahakama kwa
ushirikiano aliopewa tangu alipoteuliwa kuhudumu katika Kanda ya Dodoma tarehe
01 Aprili, 2018 na amejifunza vitu vingi.
“Katika Mhimili huu watu wote tunategemeana, kila mtu ana nafasi yake wakati
wa kutekeleza wajibu kazini awe Mlinzi, Dereva, Muhudumu, Karani na yoyote
katika kada zote.
“Mathani, bila Mlinzi kuwepo na ofisi ikaungua au mafaili yote yakaibiwa,
maana yake huduma hazitatolewa. Hivyo, nasisitiza upendo na heshima kwa kila mtu
na kumtegemea Mungu ndio nguzo kubwa katika maisha,” alisema.
Nao baadhi ya Majaji na watumishi wa Mahakama Kanda ya Dodoma waliohudhuria
hafla hiyo wamemwelezea Jaji Masaju kuwa ni mtu mwenye weledi na
anayesimamia sheria. Wamesema Jaji Masaju ametoa mchango mkubwa katika
maboresho yanayoendelea mahakamani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
hivi karibuni alimteua Jaji Masaju kuwa mshauri wa Rais kwenye masuala ya
kisheria.
Jaji Masaju alikuwa mshauri wa kisheria katika Ofisi ya Rais kabla ya
kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwaka 2009. Aliteuliwa kuwa Mwanasheria
Mkuu wa Serikali tarehe Januari 2, 2015. Aliteuliwa kuwa Jaji wa
Mahakama Kuu tarehe 1 Februari, 2018.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni