Ijumaa, 5 Mei 2023

MASHAURI YA MLUNDIKANO SASA HISTORIA KANDA YA SHINYANGA

Na. Emmanuel Oguda – Mahakama Shinyanga. 

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga imefanikiwa kumaliza mashauri ya mlundikano katika ngazi zote za Mahakama, kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama za Hakimu Mkazi isipokuwa Mahakama Kuu pekee ambapo limebakiwa na shauri moja tu linaloendelea kusikilizwa katika kikao cha mashauri ya Jinai (Criminal Session) cha Mahakama Kuu kinachoendelea wilayani Kahama.

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano ya Ofisi jana tarehe 04 Mei, 2023 aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Athuman Matuma wakati akikabidhi Ofisi ya Jaji Mfawidhi kwa Mhe. Amour Khamis ambaye amehamishiwa katika Kanda hiyo hivi karibuni.

Mhe. Matuma aliwapongeza Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga kwa kuonyesha kushirikiano na juhudi kubwa ya kufanikisha azma ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga iliyojiwekea katika kikao cha pamoja kilichofanyika mwezi Februari, 2022 ambacho kiliazimia kuwa na mashauri sifuri ya mlundikano.

“Ninayo furaha na amani kuona ninakabidhi kituo ambacho kina shauri moja tu la mlundikano ambalo kimsingi linaendelea hivi sasa na litamalizika hivi karibuni, hivyo Kanda ya Shinyanga itakuwa na mashauri sifuri kabisa, niwapongeze sana watumishi wa Kanda hii kwa juhudi, kujitoa kwa hali na mali kufanikisha kile tulichoazimia’’ alisema Jaji Matuma. 

Aidha, Jaji Matuma alimuhakikishia Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Amour Khamis kuwa, watumishi wa Kanda ya Shinyanga ni wachapakazi na watampa ushirikiano kama waliompatia alipokuwa akiongoza Kanda hiyo.

“Mhe. Amour nikuhakikishie tu, watumishi hawa ni wachapa kazi, wana nidhamu pia ni imani yangu wataendelea kukupa ushirikiano kama walionipatia mimi, niwaombe pia, tuendeleze mikakati ambayo tulijiwekea ili Kanda ya Shinyanga iendelee kuwa bora katika kutoa huduma kwa wananchi’’ aliongeza Jaji Matuma.

Kwa upande wake Jaji Mfawidhi aliyekabidhiwa Ofisi, Mhe. Amour Khamis aliwapongeza watumishi wa Kanda ya Shinyanga kwa kazi kubwa hasa kufanikiwa kumaliza mashauri ya mlundikano, Mhe. Khamis amesema kuwa, kila mmoja anayo nafasi katika kutekeleza nguzo tatu za mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa mwaka 2020/2021 – 2024/2025, hivyo kila mmoja awajibike kwa nidhamu kubwa, juhudi kubwa kutekeleza mpango Mkakati huo.

Aidha, Jaji Khamis alimpongeza aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo kwa hatua kubwa pamoja na mafanikio katika kutekeleza majukumu na kufanikiwa kutokuwa na mashauri ya mlundikano ndani ya Kanda hiyo. ‘’Mhe. Jaji Matuma, kile ambacho umekifanya nitaendelea kukienzi na kukiendeleza, pale ulipoishia wajibu wangu sasa ni kuendeleza tulipofikia ili tuwe na matokeo mazuri zaidi’’ alisema Jaji Khamis.

Hali kadhalika, Jaji Amour amewataka watumishi kumpa kushirikiano, kufanya kazi kwa bidii, nidhamu na kuwa na hofu ya Mungu, Mhe. Amour amewataka watumishi wote ndani ya Kanda ya Shinyanga kuridhika na kile wanachikipata na kuishi kulingana na kipato kwani kwa kufanya hivyo watakuwa na amani katika mioyo yao.

Pia, Jaji Khamis aliwasisitiza watumishi kuzingatia miongozo mbalimbali inayotolewa na Viongozi Wakuu wa Mahakama ya Tanzania, alimuagiza Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga Bi. Mavis Miti kuhakikisha miongozo hiyo inawafikia watumishi wa Mahakama katika ngazi zote na kuhakikisha wanaielewa na kuizingatia.

“Miongozo ya viongozi wetu wakuu wa Mahakama ya Tanzania isambazwe kwa watumishi wote kwani miongozo hiyo inalenga zaidi Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa miaka mitano ambao tunautekeleza hivi sasa’’ aliongeza Jaji Khamis.

Akiongea kwa niaba ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Shinyanga, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Seif Kulita amemkaribisha Mhe. Khamis na kuahidi kuendeleza ushirikiano kama ambavyo alipatiwa Jaji Matuma wakati wote akiwa Jaji Mafawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga. 

Mhe. Kulita amemuahidi Jaji Amour kuwa, watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga wataendelea kuchapa kazi kwa bidii, kuimarisha nidhamu pamoja na kuzuia mashauri ya mlundikano (backstopping).

“Kanda yetu ikiwa na mafanikio, kila mmoja atakuwa amechangia mafanikio hayo, hivyo ushirikiano uendelee kutolewa kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga ili atimize majukumu yake kwa ufanisi’’ alisema Jaji Kulita.

Naye Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Warsha Ng’humbu ametoa pongezi kwa Jaji Mfawidhi aliyehamishiwa Kanda ya Tabora kwa jitihada zake kuifikisha Kanda ya Shinyanga kuondoa mashauri ya mlundikano, ameahidi ushirikiano kwa Jaji Mfawidhi aliyehamia Kanda ya Shinyanga.

Kwa Upande wao, watendaji wa Mahakama katika Kanda hiyo wamemkaribisha Jaji Mfawidhi aliyekabidhiwa Ofisi na kuahidi kumpatia ushirikiano, pia wamemshukuru Jaji Mfawidhi aliyekabidhi ofisi kwa kuwa mwalimu mzuri kila alipotembelea Mahakama kuanzia Mahakama za Mwanzo hadi Mahakama za Hakimu Mkazi.

“Mhe. Matuma alikuwa mwalimu mzuri na wakati wote alipotembelea Mahakama zake, alifanya ukaguzi kwa vitendo na wote tutakubaliana kwamba alikuwa ni mwalimu mzuri na tulijifunza kupitia yeye’’ alisema Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu. Bw. Gasto Kanyairita.

         Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, Mhe. Athuman Matuma akikabidhi Ofisi kwa Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Amour Khamis wakati wa hafla ya makabidhiano iliyofanyika Mahakama Kuu-Shinyanga tarehe 04 Mei, 2023.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, Mhe. Athuman Matuma (aliyesimama) akitoa ufafanuzi wa jambo kabla ya kukabidhi taarifa ya Kanda ya Shinyanga kwa Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Mhe. Amour Khamis kwenye hafla fupi ya makabidhiano ya Ofisi ya Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga.

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania- Kanda ya Shinyanga, Mhe. Amour Khamis akiongea na watumishi mara baada ya kukabidhiwa Ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo.

       Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania- Kanda ya Shinyanga, Mhe. Seif Kulita, akiwa kwenye hafla hiyo.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania- Kanda ya Shinyanga, Mhe. Warsha Ng’humbu akizungumza jambo wakati wa makabidhiano ya Ofisi ya Jaji Mfawidhi.

  Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Bi. Mavis Miti akizungumza jambo wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi ya Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga.

     Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita akitoa neno la shukrani wakati wa hafla ya makabidhiano ya Ofisi ya Jaji Mfawidhi.




















Hakuna maoni:

Chapisha Maoni