·Msisitizo watolewa taarifa sahihi za ukaguzi Mahakama za Mwanzo
Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha
Mahakama Mkoa wa Pwani hivi karibuni ilifanya Kikao cha Menejimenti kujadili mambo mbalimbali ya kiutendani katika mustakabali mzima wa kuboresha huduma za utoaji haki kwa wananchi.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti mkoani hapa kilipokea taarifa mbalimbali, ikiwemo ukusanyaji wa maduhuri kwa kipindi cha miezi sita toka Oktoba 2022 mpaka Machi 2023.
Afisa utumishi wa Mahakama ya Wilaya Bagamoyo Isihaka Mgude ndiye aliyewasilisha taarifa hiyo kwenye Kikao hicho kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali waandamizi wa Mahakama katika Mkoa huo.
Akisoma yatokanayo na kikao kilichopita na utekelezaji wake, Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Pwani, Bw. Moses Minga alisema wamejipanga kutoa mafunzo kwa watumushi ili kuwajengea uelewa kwenye mifumo mbalimbali ya kielekroniki inayotumika mahakamani.
“Tumetenga fedha kwa ajili ya kuwapatia mafunzo Wasaidizi wa Kumbukumbu ili kuendana na kasi iliyopo, hasa katika teknolojia ambapo kuna mifumo miwili ambayo wanatakiwa kuifahamu vyema na kuitumia kwa usahihi,” alisema.
Bw. Minga aliitaja mifumo hiyo ambayo ni mfumo wa kusajili na kuhuisha mashauri(JSDS) na mfumo E-office ambapo Mahakama ifikapo mwezi June 2023 haitatakiwa kutumia karatasi katika shughuli za kimahakama.
Akizungumza katika Kikao hicho, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani, Mhe. Joyce Mkhoi aliwataka Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya kujaza taarifa zao za ukaguzi wa Mahakama za Mwanzo kwa usahihi.
Alisema taarifa za ukaguzi zinazofanywa na Mahakama za Wilaya zina mapungufu, hivyo akahimiza Mahakimu hao kujaza kwa ukamilifu kama mwongozo unavyoelekeza.
Kikao hicho cha menejimenti kilijumuisha wajumbe 16 ambapo Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya na Maafisa Utumishi walihudhuria. Kikao hicho ni moja ya vikao vinavyofanyika kila baada ya miezi mitatu.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kibaha-Pwani,
Mhe. Joyce Mkhoi
akisikiza taarifa mbalimbali katika kikao hicho.
Mtendaji wa Mahakama ya Hakimi Mkazi Pwani, Bw. Moses Minga akifurahia jambo baada ya kutoa taarifa yake ya utekelezaji.
Wajumbe wa kikao cha menejimenti cha Mahakama Pwani wakiwa katika picha ya pamoja.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni