Na Hasani Haufi – Mahakama, Songea
Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Songea, hivi karibuni iliendesha mafunzo kwa watumishi wake kuwajengea
uelewa kuhusu Mfumo wa Sema na Mahakama unaohusu upokeaji na ushughulikiaji wa
malalamiko kieletroniki (e-complaint) yanayotolewa na wananchi.
Akifungua mafunzo hayo
yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Songea, Kaimu Mtendaji wa Mahakama Kanda
ya Songea, Bi. Paulina Kapinga alieleza matumaini yake baada ya mafunzo hayo,
wao kama wapokeaji na washughulikiaji wa ndani wa malalamiko watakuwa tayari
kutoa huduma bora zaidi na haraka kwa wananchi.
“Ni imani yangu kuwa
baada ya mafunzo haya, watumishi watakuwa na uelewa wa pamoja wa namna ya
kupokea na kushughulikia malalamiko kwa njia ya kielektroniki yanayotolewa na
wananchi,” alisema.
Mafunzo hayo yalitolewa
na Afisa Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Mahakama Kuu ya Tanzania,
Kanda ya Songea, Bi. Catherine Okumu. Alieleza kuwa Mahakama ipo katika
utekelezaji wa mpango mkakati (2021/2022-2024/25), lengo ni kuhakikisha utoaji
huduma ya haki unamlenga mwananchi.
Aliwaeleza washiriki wa
mafunzo hayo kuwa katika kutekeleza malengo hayo ya kimkakati, Mahakama imeona
ni vyema kuwekeza zaidi katika matumizi ya TEHAMA ikiwemo mfumo huo wa e-Complaints.
Alifafanua namna ya
kupokea na kusajili malalamiko kutoka kwa wateja wa ndani pamoja na wateja wa
nje, huku akielezea namna ya kushughulikia lalamiko lililowasilishwa na wateja kama
linahusu taasisi au idara nyingine.
Bi. Catherine alisema
kuwa ujio wa mfumo huo wa kielektroniki unawataka watumishi wa Mahakama
kuyaishi mageuzi na matumizi ya TEHAMA wanapotekeleza majukumu yao ya kimahakama.
Mafunzo hayo yalifungwa na
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Elizabeth
Nyembele, ambaye aliwasihi watumishi wawe na utayari chanya wa kutumia mfumo
huo ili kufikia mwelekeo sahihi wa Mahakama Mtandao, ‘e-Judiciary.’
Kaimu Mtendaji wa Mahakama
Kanda ya Songea, Bi. Paulina Kapinga akizungumza wakati anafungua mafunzo kwa
watumishi wa Mahakama katika Kanda hiyo.
Afisa TEHAMA wa Mahakama Kuu
Kanda ya Songea, Bi. Catherine Okumu akitoa mafunzo kwa washiriki.
Washiriki wa mafunzo hayo
wakifatilia mada kwa ukaribu.
Washiriki wakijadiliana
baada ya kushirikishwa na mwezeshaji kutoa michango yao.
Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Elizabeth Nyembele akitoa msisitizo juu
ya mfumo huo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni