·Wafurahia kuona miundombinu ya kisasa, maboresho ya
huduma za kimahakama
Na Stanslaus Makendi na Arapha Rusheke, Mahakama Kuu Dodoma
Wanachuo kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wapatao hamsini hivi karibuni walifanya ziara ya kimasomo katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma na kupokelewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu.
Katika ziara yao, wanachuo hao walipata wasaa wa kuongea na viongozi wa Mahakama Kuu Dodoma na kuelezwa muundo na namna Kituo Jumuishi hicho kinavyotoa huduma zake kwa wananchi. Baadaye walitembelea maeneo mbalimbali ya Kituo hicho kujionea huduma zinavyotolewa.
Akiongea na wanachuo hao, Jaji Mdemu alibainisha kuwa IJC Dodoma inajumuisha Mahakama ya Mwanzo, Mahakama ya Wilaya, Mahakama ya Watoto, Mahakama Kuu na sehemu ya Mahakama ya Rufani.
Alieleza kuwa Kituo hicho kimewezesha Mahakama kuwa karibu na wadau muhimu katika mnyororo wa utoaji Haki, wakiwemo Jeshi la Polisi, Magereza, Waendesha Mashtaka, Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Uangalizi, Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Kujitegemea.
Aliendelea kubainisha kuwa Muundo wa Vituo Jumuishi umewawezesha wananchi kupata huduma za Mahakama kwa ukaribu zaidi katika jengo moja, hivyo kuwapunguzia gharama za uendeshaji wa mashauri yao mahakamani.
Kwa upande wao, wanachuo walioshiriki ziara hiyo waliushukuru uongozi wa Mahakama kwa kuwapa fursa hiyo ya kujifunza na kujionea namna huduma zinavyotolewa katika Kituo Jumuishi.
Naye Mwakilishi wa Klabu ya Mazingira IJA (Green Club) na Mbunge wa Serikali ya Chuo (IJASO), Bi. Irene Mlay alifurahia kuona mazingira safi ya Kituo hicho na kushiriki kupanda mti wa kumbukumbu katika eneo hilo.
Aliposikia kuhusu Azimio la Morogoro
la Mahakama linalolenga kuboresha mazingira, kiongozi huyo wa wanafunzi alijitolea
kuwezesha miti mbalimbali kutoka katika Klabu yao ili kushirikiana na Mahakama kuboresha
hifadhi ya mazingira.
Mwakilishi wa Klabu ya Mazingira ya Chuo hicho (Green Club) na Mbunge wa Serikali ya Wanachuo (IJASO), Bi. Irene Mlay akipanda mti katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono Azimio la Morogoro la Mahakama kuhusu uboreshaji wa mazingira.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu na sehemu ya wanachuo wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakishuhudia upandaji wa mti kama kumbukumbu ya ziara yao Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma.
(Habari hii imehaririwa na FAUSATINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni