·Hoja tano zaafikiwa kupelekwa kwenye Baraza Kuu
·Kasi utoaji elimu Divisheni ya Kazi haipimiki
Na Faustine Kapama na Mwanaidi Msekwa-Mahakama Kazi
Kikao hicho kilichofanyika katika Kituo Jumuishi cha
Utoaji Haki Kinondoni kilihudhuriwa pia na viongozi waandamizi wa Divisheni hiyo,
Naibu Msajili Mfawidhi, Mhe. Said Ding’ohi, Naibu Msajili, Mhe. Enock Cassian
na Mtendaji, Bw. Samson Mashalla.
Baada ya kufungua Kikao hicho, Mhe. Dkt. Mlyambina aliwakaribisha
wajumbe kuimba wimbo maarufu wa wafanyakazi wa ‘solidarity forever’ na baadaye
kufanya utambulisho kabla ya kumruhusu Katibu Msaidizi wa Baraza, Bw. Robert
Mchocha kusoma agenda.
Akiwakaribisha wajumbe katika Kikao hicho, Jaji Mfawidhi
aliwaomba kuwa huru kuchangia na kutoa maoni mazuri yatakayosaidia Baraza hilo
kufikia maazimio yatakayowasaidia siyo tu watumishi wa Divisheni hiyo, bali pia
wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania kwa ujumla.
“Niwashukuru wajumbe kwa kuhudhuria kwenye Kikao cha
Baraza hili. Ushiriki wenu ni muhimu sana kwani michango ya mawazo mtakayotoa
itasaidia kufikia maazimio yenye tija yatakayopelekwa kawenye Baraza Kuu siyo
kwa manufaa yetu sisi bali pia watumishi wa Mahakama kwa ujumla,” alisema.
Katika Kikao hicho kilichohudhuriwa na Katibu wa TUGHE
wa Wilaya za Kinondoni na Temeke, Bw.
Steven Wadi, hoja tano zilizochambuliwa kwa kina ziliazimiwa na wajumbe
kuwasilishwa kwenye Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania.
Kadhalika, katika Kikao hicho, Karani Mkuu, Bw. Mchocha, alitangazwa rasmi kuwa mfanyakazi
bora wa Divisheni hiyo baada ya kukamilika kwa mchakato ulioanza wiki kadhaa
zilizopita.
Mwishoni mwa mwezi Aprili, 2023, wafanyakazi wa Divisheni
hiyo walipendekeza majina matano ambayo yalipelekwa katika Menejimenti kwa
ajili ya uchambuzi wa kumpata mfanyakazi bora mmoja.
Jina la Bw. Mchocha lilichomoza miongoni mwa watumishi
waliopendekezwa baada ya wajumbe wa Menejimenti ya Divisheni ya Kazi kuchambua
sifa na vigezo vya kuwa mfanyakazi bora vilivyowekwa na TUGHE.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi,
Mhe. Dkt. Modesta Opiyo alipata nafasi ya kumtangaza mfanyakazi bora huyo kwenye
tafrija fupi iliyofanyika mahakamani hapo.
Kabla ya tafrija hiyo, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi
iliendeleza utamaduni wake wa utoaji wa elimu ya sheria kwa wadau na watumishi
wake. Tarehe 3 Mei, 2023, mada mbili muhimu za mifumo ya Teknolojia ya Habari
na Mawasiliano (TEHAMA) ziliwasilishwa.
Mada moja ya Mfumo wa Sema na Mahakama unaohusu
uwasilishaji kwa njia ya kielektoniki wa malalamiko, mapendekezo, maoni na mrejesho
kutoka kwa wananchi wa huduma zinazotolewa na Mahakama ilitolewa na Afisa
TEHAMA kutoka Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, Bw. Lazaro Sanga.
Baadaye tarehe 5 Mei, 2023 mfumo wa Tanzlii wa
kuhifadhi uamuzi unaotolewa na Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu pamoja na sheria
mbalimbali uliwasilishwa kwa viongozi na watumishi wa Divisheni hiyo na
waanzilishi wa mfumo huo, Mhe. Kifungo Kariho na Bw. Salum Tawan.
Kamati ya Elimu ya Ndani ya Mahakama Kuu ya Tanzania,
Divisheni ya Kazi, chini ya Mwenyekiti wake, Jaji wa Mahakama Kuu kutoka
Divisheni hiyo, Mhe. Katarina Mteule imekuwa ikisisitiza matumizi ya TEHAMA kwa
watumishi na wadau ili kuboresha utoaji wa huduma bora za kimahakama kwa
wananchi.
Wajumbe wa Baraza Kuu wakiimba wimbo wa 'solidarity forever' kabla ya kuendelea na kikao.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (kulia) akimpongeza Bw. Robert Mchocha kwa kuchaguliwa kuwa mfanyakazi bora wa Divisheni hiyo.
Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (katikati waliokaa) ikiwa katika picha ya pamoja na viongozi waandamizi wa Mahakama hiyo. Wengine waliokaa ni Katibu Msaidizi wa Baraza, Bw. Robert Mchocha (kushoto) na Katibu wa TUGHE wa Wilaya za Kinondoni na Temeke, Bw. Steven Wadi (kulia).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni