Ijumaa, 26 Mei 2023

WADAU WA MAHAKAMA MOROGORO WASTAAJABISHWA NA MABORESHO; WASIFU JITIHADA ZA MAHAKAMA

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

Wananchi waliofika kupata huduma katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro wamepongeza jitihada za Mhimili huo kufuatia maboresho makubwa yaliyofanyika kwa upande wa utoaji haki na miundombinu yake.

Pongezi hizo zilitolewa jana tarehe 25 Mei, 2023 wakati wa kipindi cha elimu kinachotolewa katika Kituo hicho kuanzia Jumatatu mpaka Alhamisi ya kila wiki ambapo ndani ya wiki hii mada kubwa ilikuwa ni maboresho yanayofanywa na Mahakama ikiwemo mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Akizungumza wakati wa kutoa elimu kwa wateja hao hivi karibuni, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Livin Lyakinana aliwaeleza kuwa Mahakama imeboresha mifumo yake ili kuweza kumsaidia mteja kupata haki kwa wakati.

“Sasa hivi mteja anaweza kukaa nyumbani kwake na akafuatilia kesi yake mahakamani kwa njia ya mtandao, hii inampunguzia mwananchi gharama za kulipia usafiri ili kumfikisha mahakamani” alieleza Mhe. Lyakinana.

Aidha Mhe. Lyakinana aliwaelekeza kwamba, kwa sasa Mahakama imeanzisha mfumo mpya wa ‘Sema na Mahakama’ ambao unampa mteja uhuru wa kutoa malalamiko, maoni na mapendekezo yake ili kuisaidia Mahakama kuboresha huduma zake bila kuingilia uhuru wake.

Elimu hiyo imetolewa kuanzia terehe 23 Mei, 2023 hadi tarehe 25 Mei, 2023 ambapo sanjari na kufundishwa kuhusu maboresho hayo pia walipata fursa ya kutembelea  moja ya kumbi za Mahakama ya Wazi (Open Court) zilizoko katika jengo hilo ambapo walijionea namna ukumbi huo ulivyojengwa kisasa na baada ya kuingia ndani ya ukumbi huo hawakusita kuonesha mshangao na kuimwagia sifa Serikali na Uongozi wa Mahakama kwa kuboresha miundombinu ya maeneo ya Utoaji Haki.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Livin Lyakinana 
(kulia) akitoa elimu kwa wananchi waliofika kupata huduma katika Mahakama hiyo jana tarehe 25 Mei, 2023.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Livin Lyakinana akiendelea kutoa elimu kwa wananchi (hawapo katika picha) kuhusu mada ya Maboresho ya Mahakama.
Wananchi wakimsikiliza Mhe. Lyakinana (hayupo katika picha).
Wananchi waliofika kupata huduma ya Mahakama katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki 9IJC) Morogoro wakisikiliza mada inayotolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Morogoro, Mhe. Livin Lyakinana (hayupo katika picha).

Muonekano wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro.

(Habari hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni