Alhamisi, 18 Mei 2023

WATUMISHI MAHAKAMA PWANI WANOLEWA KUHUSU MFUMO WA KURATIBU MALALAMIKO

Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha

Watumishi kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani na Mahakama ya Wilaya Kibaha waliochaguliwa hivi karibuni kuratibu mrejesho wa wananchi jana tarehe 17 Mei, 2023 wamepata mafunzo jinsi ya kuendesha mfumo wa kupokea na kushughulikia malalamiko kwa njia ya mtandao (E-Complaint). 

Mfumo huo umeanza kufundishwa toka tarehe 10 Mei, 2023 kwa Kanda ya Dar es Salam na mpaka sasa Wilaya nne za Mkoa wa Pwani zimeshaunganishwa. Watumishi waliopata mafunzo hayo ni Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala. 

Akieleza madhumuni ya mfumo huo katika mahojiano maalumu, Afisa Teknolojia Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wa Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Elicia Meena alisema mfumo huo utasaidia kupata mrejesho, maoni, mapendekezo na malalamiko kutoka kwa wananchi kadri wanavyohudumiwa. 

“Mfumo huu ni kujitathimini na kushughulikia matatizo kwa wakati, kuwa na takwimu za malalamiko, pongezi na mapendekezo ili kuboresha huduma za Mahakama,” Mtendaji wa Mahakama Mkoa wa Pwani, Bw. Moses Minga alisema.

Alieleza kuwa Mpango Mkakati wa Mahakama wa mwaka 2020 -2025 unasisitiza matumizi ya TEHAMA, hivyo mfumo wa malalamiko ni sehemu ya mpango mkakati huo.

“Katika mapinduzi ya viwanda ya kwanza mpaka ya tatu, Waafrika hatukuwemo, lakini sasa hivi katika mapinduzi ya nne ya viwanda Waafrika tumo, hivyo inabidi kila Mwafrika ajitahidi kutumia mtandao ili kwenda na mapinduzi haya,” alisema. 

Mtendaji huyo alisema mfumo huo utasaidia kupokea malalamiko mengi kwa mara moja katika Mkoa, hivyo kurahisisha utendaji kazi na kupata takwimu sahihi. Alitoa wito kwa jamii kutumia mitandao ili kuokoa muda na kupunguza gharama.

 

Mtendaji wa Mahakama Mkowa wa Pwani, Bw. Moses Minga (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Afisa TEHAMA wa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam, Bi. Elicia Meena (wa pili kushoto), Afisa Tawala Mkoa, Bi. Stumai Hoza (wa kwanza kushoto), Karani Mkuu Mahakama ya Wilaya Kibaha, Bi. Sarah Kafuko (wa kwanza kulia) na Msaidizi wa Kumbukumbu Mahakama ya Hakimu Mkazi, Bi. Zakia Ally baada ya mafunzo.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni