Na Hasani Haufi – Mahakama, Songea
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania jana tarehe 18 Mei,
2023 imefanya ziara katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea kukusanya maoni
juu ya marekebisho ya ya sheria dhidi ya makosa ya maadili ya utu.
Wajumbe wa Tume hiyo wakiongozwa na Afisa Sheria
Mwandamizi, Bi. Christina Binali walipokelewa kwa bashasha na Kaimu Jaji Mfawidhi,
Mhe. Upendo Madeha, ambaye aliahidi kuwapa ushirilikiano.
“Napenda kumshukuru Mungu kwa kufika salama, poleni
na uchovu wa safari, karibuni sana Songea. Tupo tayari kuyapokea mliyotuletea
na tutawapa ushirikiano,” alisema.
Baada ya ukaribisho huo, Mhe. Madeha aliwatambulisha
Mahakimu Wakazi waliokuwepo, wakiwemo Wafawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi na
Mahakama ya Wilaya Songea Mjini na hatimaye kumkaribisha Bi. Binali.
Akizungumza katika tukio hilo, Afisa Sheria huyo alieleza
kuwa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ni taasisi ya Serikali inayojitegemea iliyoanzishwa
chini ya Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Sura ya 171.
“Jukumu la Tume ni kupitia sheria zote za Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na kutoa mapendekezo ya kuziboresha ili kuzifanya ziendane
na mazingira yaliyopo kwa maendeleo endelevu, hivyo ninaomba sana mawazo yenu
ya kina ili kufanikisha zoezi hili,” alisema.
Tume hiyo ilikuja na dodoso la utafiti wa mapatio ya
mfumo wa sheria zinazosimamia makosa dhidi ya maadili Tanzania, ambayo ilikuwa
kama mwanga kwa wachangiaji.
Kaimu Jaji Mfawidhi aliwasilisha maoni yake, kwanza
kwa kuzungumza na kisha kutoa maoni hake kwa Tume yaliyokuwa kwenye muundo wa
maandishi.
Mhe. Madeha alieleza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kufanya marekebisho ya sheria juu ya makosa ya maadili ya utu kutokana na kuongezeka kwa makosa hayo katika jamii.
Kaimu
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Songea, Mhe. Upendo Madeha (kulia)
akimkabidhi maoni ya marekebisho ya sheria juu ya makosa dhidi ya maadili ya
utu Afisa wa Sheria Mwandamizi, Bi. Christina Binali.
Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda
ya Songea, Mhe. Upendo Madeha (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya
pamoja na wajumbe kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni