Na Yusufu Ahmadi- IJA Lushoto.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Dkt. Gerald Ndika amewaomba Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani walioteuliwa hivi karibuni kuichukulia nafasi hiyo kwa uzito unaostahili, kwani jamii ina matarajio makubwa kutoka kwao.
Mhe. Dkt. Ndika, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama alitoa wito huo hivi karibuni alipokuwa anafunga mafunzo elekezi yaliyokuwa yanatolewa kwa Majaji hao katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA).
"Muichukulie nafasi hii kwa uzito wa hali ya juu, tukumbuke majukumu yetu ni makubwa na matarajio ya jamii kwetu na Mahakama ni makubwa mno," alisema.
Mhe. Dkt. Ndika aliwasihi Majaji hao kutoa haki bila woga, chuki na upendeleo na kuzikabili changamoto zilizo mbele yao kwa nia moja.
"Dira yetu kama ambavyo imekuwa siku zote ni kutoa haki bila woga, chuki na upendeleo huku tukiongozwa na misingi ya haki na usawa pamoja na heshima. Hivyo, tuzikabili changamoto zilizo mbele yetu kwa nia moja," alisisitiza.
Kabla ya kufunga mafunzo hayo, Jaji Ndika aliwasilisha mada mbili na kuzungumzia umuhimu wa mtu kuwa na hamasa (passion) katika kufanya jambo. Alisema hamasa ni kichocheo katika kulifanya jambo kwa ufanisi na kupata matokeo bora.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mahakama ya Tanzania na kuendeshwa na Chuo cha IJA yalifunguliwa tarehe 12 Juni, 2023 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Majaji hao wapya sita waliopatiwa mafunzo hayo ni wale walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 18 Mei, 2023 na kuapishwa tarehe 23 Mei, 2023 katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Majaji hao ni Mhe. Zainab
Goronya Muruke, Mhe. Leila Edith Mgonya, Mhe. Amour Said Khamis, Mhe. Dkt.
Benhajj Shaaban Masoud, Mhe. Gerson John Mdemu na Mhe. Agnes Zephania Mgeyekwa.
Waliungana na Jaji mwingine wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sam Mpaya Rumanyika
ambaye alikuwa hajapata mafunzi hayo.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt Gerald Ndika (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo. Wengine waliokaa ni Mkuu wa Chuo na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo (kushoto) na Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Patricia Ngunguru (kulia). Waliosimama kutoka kulia, ni Mhe. Jaji Agnes Zephania Mgeyekwa, Mhe. Dkt. Benhajj Shaaban Masoud, Mhe. Leila Edith Mgonya, Mhe. Zainab Goronya Muruke, Mhe. Sam Mapaya Rumanyia, Mhe. Amour Said Khamis na Mhe. Gerson John Mdemu.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni