Jumatatu, 19 Juni 2023

WASHITAKIWA 13 KESI YA UGAIDI WAACHIWA HURU

Na Seth Kazimoto, Mahakama Arusha.

Mahakama Kuu Arusha imewaachia huru washitakiwa wote 13 waliokuwa wanakabiliwa na kesi ya jinai iliyohusisha matukio mbalimbali ya kigaidi yaliyotokea katika Mkoa wa Arusha katika vipindi tofauti kati ya mwezi Januari na Julai 2014.

Uamuzi huo umetolewa Ijumaa tarehe 16 Juni, 2023 na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Arusha, Mhe. Emmanuel Ngigwana katika shauri la jinai namba 65/2022 baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha tuhuma dhidi ya washitakiwa hao bila kuacha shaka yoyote, kama inavyotakiwa kisheria.

“Jukumu la kuondoa shaka yoyote ni la upande wa mashtaka ambao umeshindwa kuthibitisha tuhuma dhidi ya washtakiwa bila kuacha shaka. Kwa hiyo, Mahakama hii inawaachia huru washtakiwa wote katika shauri hili,” Jaji Ngigwana alisema.

Akisoma kukumu kwa ufupi, Jaji Ngigwana alisema kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka una mashaka mengi na hivyo kushindwa kuthibitisha tuhuma dhidi ya washtakiwa.

Aliendelea kueleza kuwa katika mashahidi wote 14 wa Jamhuri, hakuna hata mmoja aliyesema kuwa aliona kwa macho watuhumiwa wakirusha bomu kwa wahanga wa matukio ya milipuko ya mabomu.

“Kadhalika, hakuna shahidi aliyeona washtakiwa wakitoa fedha ili kufadhili vitendo vya kigaidi. Kwa mfano, mshtakiwa (mmoja) alituhumiwa kutoa fedha kufadhili ugaidi, lakini upande wa mashtaka haukuleta maelezo ya onyo mahakamani kuthibitisha tuhuma hiyo,” alisema.

Vilevile, Jaji Ngigwana alisema kuwa hakuna shahidi wa Jamhuri aliyesema kuwa aliwaona washtakiwa wakiwa kwenye vikao vya kupanga kufanya vitendo vya kigaidi.

Aliendelea kueleza kuwa ushahidi wa Jamhuri uliegemea ukiri (confession) kwa baadhi ya washitakiwa wakiwa katika Kituo cha Polisi, ukiri wa washtakiwa wenza na ushahidi wa kusikia.

Jaji alisema kwamba ushahidi wa ukiri ulioletwa na upande wa Jamhuri una mashaka kwa kuwa haukidhi vigezo vinavyotakiwa kisheria.

“Mtu akikiri kosa, akiri viini vyote vya kosa na ukiri ujieleze wenyewe, ukiri uwe huru bila kulazimishwa au kushawishiwa na kwamba mtoa maelezo lazima aonywe juu ya maelezo yake anayotoa,” Jaji Ngigwana alifafanua.

Mhe. Ngigwana alieleza kuwa ushahidi wa ukiri wa watuhumiwa wenza ulipingwa na washtakiwa wengine, hivyo maelezo yaliyopingwa peke yake hayawezi kutumika kumtia mtuhumiwa hatiani. “Maelezo pekee ya mtuhumiwa mwenza hayatoshi kumtia mtu hatiani,” aliongeza.

Aidha, Jaji huyo alieleza pia kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuleta maelezo ya onyo ya washtakiwa wote 13 kama ilivyoelezwa kwenye hati ya mashtaka na badala yake ilileta maelezo ya onyo ya washtakiwa wanne tu.

Kuhusu ushahidi wa kusikia ulioletwa na upande wa mashtaka, Jaji alieleza kuwa ushahidi wa aina hiyo hauna thamani (Value) mahakamani.

Katika shauri hilo, washitakiwa walikuwa wanakabiliwa na mashataka mbalimbali, ikiwemo kufanya jaribio la kuua, kushiriki katika vikao vya kupanga vitendo vya kigaidi, kufanya vitendo vya kigaidi, kutoa fedha kufadhili vitendo vya kigaidi na kutotoa taarifa za mipango ya kutekeleza vitendo vya kigaidi.

Washitakiwa wote walikana tuhuma dhidi yao. Washtakiwa hao walikuwa Yahaya Mpemba, Yusuph Huta, Abashari Omari, Kassim Ramadhani, Jafari Lema, Abdul Humud, Hassan Mfinanga, Anuwar Hayer, Yusuph Athuman, Abdul Hassan, Swalehe Hassan na Rajabu Abdallah.

Upande wa utetezi ulikuwa na Mawakili wasomi 13 walioongozwa na Upendo Msuya na Fridolin Bwemelo. Upande wa Jamhuri ulikuwa na Mawakili wa Serikali kadhaa, akiwemo Grace Madikenya.


Mhe. Emmanuel Ngigwana. 

Washtakiwa wakiwa na Mawakili wao baada ya kuachiwa huru katika shauri lao la ugaidi lililokuwa likiwakabili katika Mahakama Kuu Arusha. Aliyeshika joho mkononi ni Wakili Msomi Upendo Msuya aliyeongoza jopo la Mawakili wa upande wa utetezi.

 (Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama, Dar es Salaam)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni