Na Stephen Kapiga-Mahakama Mwanza
Mahakama
Kanda ya Mwanza hivi karibuni ilifanya kikao cha kusukuma mashauri ya jinai kwa
Mikoa ya Mwanza na Geita na kuondoka na azimio la kuunda Kamati maalumu ya
kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu jinai ili kupambana na
angozeko la makosa ya aina hiyo.
Kikao
hicho kiliongozwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza,
Mhe. Dkt Ntemi Kilekamajenga na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali. Wakati wa kikao
hicho, Mhe. Kilekamajenga alimteua Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi (RCO)
Mkoa wa Mwanza, Mrakimu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Yesayua Sudi kuwa Mwenyekiti
wa Kamati hiyo.
RCO
Sudi atasaidiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza,
Mhe Chiganga Tengwa pamoja na wajumbe wengine kutoka taasisi za dini, ofisi ya
Ustawi wa Jamii na ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Mwanza.
“Ndugu
zangu, Kamati hii itasaidia kutoa elimu kuhusu masuala mbalimbali yanayohusiana
na makosa ya jinai ili kusaidia kupata ushirikiano kutoka kwa jamii na kuondoa dhana
kuwa Mahakama imekuwa ikikosea inapomwachiwa huru mshitakiwa kutokana na ushahidi
kutojitosheleza,” alisema wakati anazungumza na wajumbe wa kikao hicho.
Jaji
Mfawidhi alibainisha kuwa Kamati hiyo inayojumuisha viongozi wa dini inategemea
kutoka elimu kila eneo kwenye mikusanyiko ya watu, kuwaeleza madhara ya kutenda
vitendo vya jinai na umuhimu wa jamii kushirikiana na vyombo vya upepelezi ili
kuwezesha haki kupatikana kwa wakati.
Jaji
Mfawidhi ameshauri kuwa ni vizuri zikatumika njia mbalimbali ili kuzuia mauaji
katika Kanda ya Mwanza kwani gharama za kuendesha mashauri ya aina hiyo ni
kubwa na mzigo kwa Serikali.
“Mpaka
kufikia tarehe 16 Juni, 2023 kuna mashauri 175 ya mauaji, hivyo kuyaendesha
yote ni gharama kubwa kwa Serikali. Mbali na kuunda Kamati hii ni vizuri kutumia
njia zingine kuzuia makosa ya mauaji ili kuokoa gharama za kuendesha mashauri
ya aina hiyo,” alisema Mhe. Dkt Kilekamajenga.
Mapendekezo
ya kuunda Kamati hiyo yalitolewa na wajumbe wa kikao hicho baada ya kubaini
kuwa makosa mengi yamekuwa yakitendeka kutokana na baadhi ya watu kukosa elimu
ya uelewa pamoja na hofu ya Mungu.
Awali,
akisoma taarifa ya mashauri kwa wajumbe wa kikao hicho, Kaimu Naibu Msajili wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. Monica Ndyekobora alieleza kuwa kasi ya
umalizaji wa mashauri imeongezeka kutoka 382 tarehe 13 Oktoba 2022 hadi kufikia
mashauri 252 kwa tarehe 16 Juni 2023.
Alisema
jumla ya mashauri 163 yalisajiliwa kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni 15,
2023 na yaliyoamuliwa yalikuwa 236, hivyo kuifanya Mahakama hiyo kuwa na
kiwango bora cha kasi ya umalizaji wa mashauri kwa asilimia 150.
Kaimu
Naibu Msajili alieleza kuwa mlundikano wa mashauri kwa upande wa Mahakama Kuu katika
Kanda hiyo umepungua kutoka asilimia 12 hadi kufikia asilimia 5.15 kwa tarehe
15 Juni, 2023.
Alisema
kuna jumla ya mashauri mlundikano 33 kwa Mahakama zote za Kanda ya Mwanza na wameweka
mikakati ya kuyamaliza ifikapo mwezi Septemba 2023.
Kuhusu matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Mhe. Ndyekobora alisema Mahakama za Kanda ya Mwanza zimeendesha jumla ya mashauri 117 kwa njia ya “video conference” kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Juni 2023, hatua inayoonesha kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yanaendelea vizuri.
Katibu
wa kikao cha kusukuma mashauri ya jinai kwa Mahakama, Kanda ya Mwanza, ambaye
ni Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Mwanza, Bi. Bibiana Kileo (kushoto) akisoma muhtasari
wa kikao kilichopita kwa wajumbe. Katikati ni Mwenyekiti wa kikao hicho, ambaye
pia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. Dkt Ntemi
Kilekamajenga.
Sehemu
ya wajumbe (juu na chini) wakiwa katika kikao cha kusukuma mashauri ya jinai kilichofanyika kwenye
ukumbi wa mikutano wa jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza.
Katibu
wa kikao cha kusukuma mashauri ya jinai, Bi. Bibiana Kileo kutoka Ofisi ya Taifa
ya Mashtaka Mkoa wa Mwanza akifafanua jambo.
Mkuu
wa Gereza la Butimba Mwanza, Mrakimu Mwandamizi wa Magereza (SSP) Deogratias
Maguza akichangia jambo wakati wa kikao cha kusumuma mashauri ya jinai.
Mkuu
wa Upelelezi wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Mrakimu Mwandamizi wa Polisi (SSP)
Yesaya Sudi (aliyesimama) akichangia na kufafanua jambo wakati wa uwasilishaji
wa maoni mbalimbali kutoka kwa wajumbe wa kikao cha kusukuma mashauri ya jinai.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni