Alhamisi, 22 Juni 2023

WAKUU WA MIKOA NA WILAYA WAOMBWA KUIKUMBUKA MAHAKAMA KATIKA MIPANGO YA MAENDELEO

 Na Lydia Churi na Aidan Robert-Kigoma

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaomba wakuu wa mikoa na wilaya kuikumbuka Mahakama ya Tanzania katika mipango ya maendeleo hususan mpango wa kusogeza mkongo wa taifa wa Mawasiliano kwenye maeneo yao.

Akizungumza na Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama katika mkoa wa Kigoma na wilaya zake Tarehe 20 Juni, 2023 mkoani humo, Mwenyekiti huyo wa Tume amesema kukosekana kwa mawasiliano ya mtandao kwenye majengo ya Mahakama husababisha shughuli za Mhimili huo kukwama kwa kuwa Mahakama ya sasa inatumia mifumo mbalimbali ya Tehama ili kurahisisha kazi ya utoaji haki.

“Majengo mapya ya Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini bado hayajaunganishwa kwenye mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, yatakapounganishwa yatasaidia mashauri kusikilizwa kwa haraka kwa njia ya Video”, alisema Jaji Mkuu.

Alisema wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ni wadau muhimu hivyo hawana budi kuielewa Mahakama inavyotekeleza jukumu lake la msingi la utoaji wa haki.

Alisema madhumuni ya Makamishna wa Tume kufanya ziara katika mikoa ya Kigoma na Tabora ni pamoja na kukutana na wajumbe wa Kamati za Maadili wa ngazi ya mkoa na wilaya. Aliongeza kuwa jukumu kubwa la wajumbe hao ni kusimamia nidhamu na maadili ya Maafisa Mahakama.

“Ninyi ni ramani inayotusaidia kuchora picha ya maadili kwa nchi nzima kupitia taarifa zenu mnazoziwasilisha kila miezi mitatu. Mnaiwakilisha Tume katika masuala ya nidhamu kwenye maeneo yenu”, alisema Prof. Juma.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Bw. Thobias Andengenye alisema Serikali mkoani Kigoma itaendeleza ushirikiano wake na Mhimili wa Mahakama na kusaidia kutatua baadhi ya changamoto zilizo ndani ya uwezo wake.

“Tutafanya kila tuwezalo kuilea Mahakama pasipo kuingilia uhuru wake ili tulinde heshima ya Mhimili huu muhimu”, alisema Mkuu wa Mkoa wa Kigoma

Akitoa neno la shukrani kabla ya kumalizika kwa Mkutano huo, Mkuu wa Mkoa  aliishukuru Mahakama kwa kusogeza huduma za utoaji haki mkoani Kigoma hususan kuanzisha na kujenga jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma pamoja na Mahakama nyingine za wilaya.

Makamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wameanza ziara ya kikazi ya siku nne katika mikoa ya Kigoma na Tabora kwa lengo la kuitangaza Tume pamoja na kuziimarisha Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (Mwenye tai nyekundu) akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Thobias Andengenye (kushoto kwake) pamoja na Makamishna wa Tume na Viongozi wa Mahakama ya Tanzania alipomtembelea Mkuu huyo wa Mkoa ofisini kwake wakati wa ziara ya Tume mkoani humo. 
Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Kigoma alipowasili kwenye Mahakama hiyo kuzungumza nao. Kushoto ni Naibu Katibu wa Tume (Ajira) Bi. Enziel Mtei.

Makamisna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wakiwa kwenye Mkutano wa Tume na Wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa wa Mahakama ngazi ya Mkoa na wilaya za Kigoma. Kulia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald Ndika akifuatiwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Mustapher Siyani. Wa pili kushoto ni Kamishna Bahame Tom na kushoto ni Kamishna Dosca Mutabuzi.

Watumishi wa Mahakama Kanda ya Kigoma wakiwa kwenye Mkutano wa Tume  

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Kigoma Mhe. Lameck Mlacha wakifuatilia Mkutano wa Tume.

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni