Alhamisi, 22 Juni 2023

MAHAKAMA SINGIDA, WADAU WAWEKA MIKAKATI KUPUNGUZA MLUNDIKANO WA MASHAURI

Na. Eva Leshange, Mahakama Singida

Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida hivi karibuni ilikutana na wadau kujadili na kuweka mikakati mbalimbali ili kuondoa mlundikano wa mashauri yaliyopo katika masjala kwenye Mahakama hiyo.

Kikao hicho ambacho kiliongozwa na Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe Ushindi Swallo kilihudhuriwa na Mahakimu Wafawidhi wa Mahakama za Wilaya Manyoni, Iramba na Singida, wakuu wa taasisi za Serikali katika Mkoa, wakiwemo TAKUKURU, Magereza, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Mkuu wa Upelelezi wa Polisi na Mganga Mkuu.

Katika kikao hicho, wadau waliendelea kusisitiza kuongeza kasi ya umalizaji wa mashauri, kuwa na maahirisho mafupi mafupi na kutoa kipaumbele katika usikilizaji wa kesi ambazo zilifutwa na kufunguliwa upya, huku upande wa upelelezi ukihimizwa kukamilisha upelelezi kabla ya kuzipeleka tena mahakamani.

Baadhi ya mikakati iliyowekwa katika kikao hicho inajumuisha Mahakimu kuwajibika ipasavyo, kuwa na vikao maalumu vya kusikiliza mashauri ya mlundikano kila baada ya miezi mitatu na vibali vya kesi, hasa ambazo zitaanza kusikilizwa Julai 2023 hadi Septemba 2023 viandaliwe ili kuepuka ucheleweshaji.

Mikakati mingine ni kutoa elimu kwa mahabusu, hasa uelewa wa sheria mbalimbali na vifungu vyake kuepuka malalamiko, matumizi ya njia mbadala kwa wale wenye vifungo vidogo, huku Magereza wakishauriwa kupunguza msongamano kwa kuhamishia wafungwa kwenye Magereza yenye nafasi.

Aidha, Kikao hicho kimeuhimiza upande wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kufuata utaratibu wa kupeleka wito (summons) kwa wakati kwa wahusika na kuhakikisha upatikanaji wao kabla ya kuandikwa wito huo.

 





Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Mhe. Ushindi Swallo (katikati) akieleza jambo katika kikao hicho. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Singida, Bw. Hussein Mkenyi ambaye alikuwa Katibu wa kikao na wa kwanza kulia ni Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Bw. Yusuph Kasuka.

Sehemu ya wajumbe (juu na chini) wakifuatilia mada katika kikao hicho.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni