Alhamisi, 22 Juni 2023

MAHAKAMA YAONGEZA WIGO UPATIKANAJI WA HAKI KWENYE MAHAKAMA ZA MWANZO NCHINI

 Na Lydia Churi- Kigoma

Mahakama ya Tanzania imeongeza wigo mpana zaidi wa upatikanaji wa haki kwa kuanzisha utaratibu unaowezesha Mawakili na Waendesha Mashtaka kuwawakilisha wananchi wenye mashauri kwenye Mahakama za Mwanzo nchini.

Akizungumza na Wadau wa Mahakama kwenye Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama uliofanyika jana mkoani Kigoma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume hiyo Mhe. Mustapher Siyani amesema kupitia mabadiliko ya Sheria, Mawakili na Waendesha Mashtaka sasa wanaweza kuwawakilisha wananchi wenye mashauri katika Mahakama za Mwanzo.

Alisema mabadiliko hayo ya Sheria yamepanua dhana ya haki kwa kuongeza fursa ya wananchi wenye mashauri kuwakilishwa na wanasheria kwenye Mahakama za Mwanzo na kwamba ni utaratibu mpya ambao haukuwahi kuwepo nchini.

Kamishna huyo wa Tume alisema ili kusaidia utekelezaji wa suala hili, tayari kanuni zimeshatungwa na zinatumika na kanuni hizo zinawataka Mawakili na Waendesha Mashtaka kutoa ahadi ya utayari wa kuendesha shauri kwenye Mahakama za Mwanzo pale wanapoajiriwa na wateja wao.

“Kama Mkurugenzi wa Mashtaka au mtu yeyote aliye chini yake ataona kuna umuhimu shauri kuendeshwa na Mwendesha Mashtaka ataijulisha Mahakama kwa Maandishi”, alisema Jaji Kiongozi.

Alisema Tume na Mahakama inatarajia kuwa uwepo wa Mawakili na Waendesha Mashtaka kwenye Mahakama za Mwanzo kutaongeza kasi ya upatikanaji wa haki nchini. Alisema haitarajiwi Maafisa hawa wa Mahakama kuhamishia mbinu za kiufundi kwenye Mahakama za Mwanzo kwa lengo la kuchelewesha mashauri kumalizika.

Jaji Kiongozi alisema Mawakili na Waendesha Mashtaka wanapaswa kuelewa historia, mazingira na mchango unaotolewa na Mahakama za Mwanzo katika upatikanaji wa haki nchini na hivyo kuzisaidia kutimiza wajibu wake. Alieleza kuwa  Mahakama hizi zinasimamia mashauri kwa wananchi takribani asilimia 70.    

Katika hatua nyingine Jaji Kiongozi ametoa wito kwa wananchi wenye mashauri mahakamani na mashahidi kutoa ushirikiano na ushahidi wa kweli bila ya kuipotosha Mahakama.

Alisema mashauri yamekuwa yakichelewa kumalizika mahakamani kutokana na mashahidi kutokufika. Akitolea mfano wa mashauri yanayohusu udhalilishaji hususan ubakaji na Ndoa za Utotoni, Jaji Kiongozi amesema baadhi ya mashauri hayo huishia kufutwa kutokana na mashahidi kutoonekana mahakamani na kuiachia lawama Mahakama.

Alisema wananchi ni wadau muhimu wa Mahakama hivyo wanao wajibu wa kisheria wa kutoa taarifa Polisi kuhusu makosa ya jina pale wanaposhuhudia yakitendeka, wana mamlaka ya kumkama mhalifiu na kumfikisha kituo cha polisi na kutoa Ushahidi wa kweli kwa makosa waliyoshuhudia yakitendeka.

Kuhusu uwepo wa Mawakili feki au vishoka, Jaji Siyani amesema wanaofanya hivyo watambue kuwa ni kosa la jinai na pia wanashusha hadhi na sifa nzuri ya taaluma ya Sheria nchini.

Alisema ni wajibu wa wadau wote wa Mahakama kuisadia Mahakama kwa kuhakiki sifa za Mawakili wanaofika Mahakamani kupitia mfumo wa E-Wakili unaowezesha kumtambua Wakili kwa majina yake au namba yake. Mfumo huu unapatikana kwa kutumia simu ya kiganjani. Amewataka Mawakili kujenga utamaduni wa kutambuana kabla ya kuingia mahakamani kwa kutumia mfumo huo.

Tume ya Utumishi wa Mahakama imekamilisha ziara yake katika mkoa wa Kigoma na itaendelea mkoani Tabora. Ziara ya Tume inalenga wajumbe wake kukutana na wajumbe wa Kamati za Maadili ya Maafisa Mahakama ngazi ya Mkoa na wilaya pamoja na wadau wa Mahakama ili kuimarisha utendaji kazi wa Mahakama ya Tanzania.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani akizungumza wakati wa Mkutano kati ya Wadau wa Utoaji haki na Tume jana mjini Kigoma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani akizungumza wakati wa Mkutano kati ya Wadau wa Utoaji haki na Tume jana mjini Kigoma.

Sehemu ya Wadau wa utoaji haki mkoani Kigoma wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Tume ya Utumishi wa Mahakama.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni