Na Eunice Lugiana-Mahakama, Kibaha
Wadau wa haki
jinai katika Mkoa wa Pwani wameomba kila ofisi kutenga fedha zitakazosaidia kuwezesha
upelelezi kufanyika kwa haraka kwenye mashauri yanayofunguliwa mahakamani.
Maombi hayo yemetolewa
na wadau hao kwenye kikao cha kusukuma mashauri katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Pwani kilichofanyika leo tarehe 22 Juni, 2023.
Akizungumza katika
kikao hicho, Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Mhe.
Joyce Mkhoi alisisitiza kila ofisi ya mdau kutenga bajeti kwa ajili ya mashihidi
ili kuepuka ucheleweshaji wa mashauri.
Naye Mkuu wa Upelelezi
Mkoa, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi Areiki Mkwaya, alisema upelelezi umekuwa
ukichelewa kukamilika kwa haraka kutokana na umbali na upatikanaji wa mashahidi.
“Kumekuwa na
changamoto kubwa ya mashihidi, ikiwemo kutopatikana kutokana na sababu
mbalimbali kama kuhama, hali inayowalazimu kutumia pesa zao binafsi kufuatilia
mashahidi hao kwa vile hakuna fungu linalotengwa kwa ajili hiyo,” alisema.
Akichangia katika
kikao hicho, Mrakibu Msaidizi wa Magereza Mohamed Shegwando aliwapongeza wadau wa haki jinai kwa kutekeleza majukumu yao kwa
ufanisi, maana wafungwa na mahabusu wamepungua.
“Hii inaonyesha Mahakama
ikishirikiana na wadau kazi nzuri inaweza kufanyika na kupunguza mlundikano katika
Magereza,” alisema na kuomba Maafisa Ustawi wa Jamii kutembelea Magereza ili
kutatua changamoto za mahabusu na wafungwa.
Kwa upande wake, Afisa
Ustawi wa Jamii, Bi. Matrida Zakaria alisema ulinzi na usalama kwa mtoto iwe ajenda
ya kila kikao cha kusukuma mashauri, kwani watoto wengi hufanyiwa ukatili na
watu wa karibu katika familia.
Alimwomba kila mjumbe kuwa mlinzi wa mtoto,
haijalishi kama ni wake au wa jirani. “Naomba wajumbe wa kikao hiki tuwe walezi
na walinzi kwa watoto. Tukiongea na watoto wetu tuwafundishe tabia njema na
kuwalinda, kwa kufanya hivyo tutaiokoa jamii yetu,” alisema.
Kabla ya kuahirishwa, kikao hicho kilitoka na maazimio kuwa upande wa mashtaka, wakishirikiana na wadau wote wa haki jinai kuchambua mashahidi kwa kina kabla ya kuleta kesi mahakamani ili kuokoa muda wa Mahakama pamoja na fedha za Serikali.
Waendesha Mashkata kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Pwani wakiwa kwenye kikao hicho.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni