Ijumaa, 23 Juni 2023

TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA YATEMBELEA MAHAKAMA YA WILAYA YA UVINZA KIGOMA

Na Aidan   Robert- Mahakama, Kigoma

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi wa Mahakama ya Wilaya ya Uvinza, iliyopo mkoani Kigoma kuendelea kufanya kazi wa uwajibikaji, weledi, na kuzingatia maadili ya Utumishi wa Mahakama.


Akizungumza hivi karibuni wakati Tume hiyo ilipotembelea Mahakama hiyo, Jaji Mkuu amesema  lengo la ziara hiyo mahakamani hapo ni kutembelea miradi iliyoisha na inayoendelea ili kuweza kuona, kujifunza na kusikiliza changamoto ambazo zinawakabili watumishi wa Mahakama. 


 “Mkoa wa Kigoma ni miongoni mwa Mikoa ambayo kwa muda mrefu imekuwa na Mahakama chache, hivyo kuchelewesha upatikanaji wa haki,ninawaomba viongozi na watumishi wa Mahakama Kigoma kuendelea kuboresha huduma kila mmoja katika eneo lake  hii ndio silaha ya kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania,” anasema Jaji Mkuu.


Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Uvinza, Mhe. Misana Majula akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama  hiyo mbele ya Tume hiyo, amesema tangu  ilipoanzishwa, mashauri yaliyofunguliwa mahakamani hapo ni  175, mashauri 102 yameamuliwa na kubakiwa na mashauri 73.  


Ameongeza kwamba Mahakama za Mwanzo zinazosimamiwa na Mahakama hiyo nazo zimepokea mashauri 550, na kusikiliza mashauri 533, na kubakiwa na mashauri 17 tu. Mashauri hayo yametoka katika Mahakama za Mwanzo nne zinazofanya kazi mpaka sasa.

“Lengo la kusogeza huduma za kimahakama kwa wananchi limefanikiwa kwa asilimia 100 katika   wilaya hiyo,” anasema Hakimu huyo.

Tume hiyo ilipongeza maboresho hayo na kuahidi kushughulikia mapungufu ya watumishi na vitendea kazi vya mahakama zote mpya, sambamba na uboreshaji ya maslahi ya watumishi.


Mahakama hiyo imeanzishwa tarehe 28, Oktoba 2022, kupitia Tangazo la Serikali Namba 616/2022. Ilianza kupokea na kusikiliza mashauri kwanzia tarehe 02 Novemba, 2022, na inasimamia Mahakama za Mwanzo sita. Aidha mpaka sasa Mahakama hiyo ina jumla ya watumishi 15 wa kada mbalimbali, wakati mahitaji halisi ni watumishi 45. Hivyo ina upungufu wa watumishi 30 ambao ni sawa na asilimia 66.67. 

 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma, na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama akiweka saini kwenye kitabu cha wageni katika Ofisi ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya Uvinza  mara baada ya kuwasili mahakamani.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia) ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama akifafanua jambo kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma mara baada ya kuwasili katika  Mahakama ya  Wilaya Uvinza. 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma,(kulia) akisikiliza kwa makini maelezo ya awali ya ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Uvinza, lilipo mkoani Kigoma, kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel, ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Kigoma. Mhe. Lameck Mlacha.

Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (kulia) ambaye pia ni Kamishna Tume ya Utumishi wa Mahakama akiteta jambo na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, ambaye pia ni Katibu wa Tume hiyo, mara baada kuwasili  katika Mahakama ya Wilaya ya  Uvinza.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahimu Hamis Juma (katikati), ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama akiwa katika picha ya pamoja na makamishna wa Tume hiyo,(wa nne kushoto) ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Kigoma.Wengine ni viongozi wa Mahakama.

(Picha na Aidan  R0bert -Mahakama, Kigoma)

(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo) 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni