Jumapili, 25 Juni 2023

TUME YA UTUMISHI WA MAHAKAMA YAKAGUA UKARABATI WA JENGO LA MAHAKAMA KUU TABORA

 Na Amani Mtinangi- Mahakama Kuu Tabora

Wajumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama wakiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma wameamaliza  ziara ya siku mbili mkoani Tabora kuanzia Tarehe 22 Juni, 2023.

Katika ziara hiyo, Mwenyekiti huyo aliambatana na Katibu wa Tume hiyo ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel pamoja na Makamishna wa Tume hiyo pamoja na viongozi waandamizi wa Mahakama ya Tanzania.

Katika Mkutano wa Tume na watumishi wa Mahakama Jaji Mkuu alipongeza kazi kubwa na nzuri inayoendelea kufanywa na watumishi wa Mahakama mkoani Tabora licha ya ukubwa wa Mkoa wa Tabora na changamoto za kijiografia zilizopo. Alieleza kuwa watumishi hao wamekuwa tayari kukabiliana na kuzitatua changamoto hizo ili kupata matokeo kusudiwa.

Akizungumzia uboreshaji wa huduma za Mahakama, Jaji Mkuu alisema kuwa maboresho ni juu ya matokeo ya kazi katika kukidhi matakwa ya wateja wa Mahakama na siyo ubora wa miundombinu pekee.

“Maboresho yaliyofanyika siyo ya ujenzi wa majengo ya Mahakama tu bali yake ni utoaji wa huduma bora katika Mahakama zetu, hayo ndiyo matunda wananchi wanayoyataka na ni mahitaji halisi ya wateja wetu”, alisema Jaji Mkuu.

Mwenyekiti huyo wa Tume pia amesisitiza umuhimu wa watumishi wa ngazi zote kujiendeleza kielimu ili kuendana na mabadiliko makubwa yanayoendelea katika karne ya 21 na kujifunza jinsi ya kukabiliana na msongo wa mawazo unaotokana na kazi za kimahakama.

Naye Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora Mhe. Athumani Matuma Kirati ameeleza kuwa Mahakama ya Tanzania kuanzia mwezi Mei 2023, imefanya mpango kabambe wa kumaliza mashauri ya mlundikano na kumaliza jumla ya mashauri mlundikano 63 yaliyokuwepo na kujikita katika mikakati ya kutozalisha mashauri ya muda mrefu.

Alieleza kwa sasa Mahakama Kuu kanda ya Tabora pamoja na Mahakama zilizo chini yake hazina mashauri ya mlundikano na kusifu ushirikiano wa watumishi na wadau wote wa Mahakama kwa kazi nzuri waliyoifanya kufanikisha umalizikaji wa mashauri hayo.

“Mhe. Jaji Mkuu, tangu mwezi Mei mwaka huu tumekuwa na kampeni ya kumaliza mashauri ambapo tumemaliza mashauri yote 63 ya mlundikamo yaliyokuwepo. Kazi hiyo haikuwa rahisi kusingekuwepo ushirikiano baina ya watumishi na wadau wa Mahakama,” Alisema Jaji Matuma.

Alifafanua kuwa kasi ya umalizaji wa mashauri ya mauaji ni ya kuridhisha mathalani kwa kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba 2022 jumla ya mashauri 115 yaliingia kwenye vikao ya yote kumalizika.

Aidha, baada ya kumalizika kwa Mkutano huo, wajumbe walipata fursa ya kutembelea na kukagua Mradi wa Upanuzi na Ukarabati Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora.

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (Mwenye tai nyekundu) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa mbalimbali wa Tume Mahakama ya Tanzania baada kukagua jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.

 

Jaji Mkuu wa Tanzania na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisaini kitabu cha wageni alipotembelea na kukagua jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Tabora.

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni