Na Lydia Churi-Tume ya Utumishi wa Mahakama-Tabora
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama
Mhe. Mustapher Siyani ametoa wito kwa jeshi la Polisi nchini kuchukua nafasi
yake ya kulinda amani kwa kuzuia uvunjifu wa amani wakati wa utekelezaji wa
amri za Mahakama pale uhitaji huo unapojitokeza.
Akizungumza
wakati wa Mkutano wa Tume na wadau wa utoaji haki mkoani Tabora, Jaji Kiongozi alisema
kwa kawaida mchakato wa utoaji haki kwenye mashauri ya madai, hauishii kwenye
hukumu kwa kuwa amri mbalimbali zinazotelewa na mahakama zinapaswa kutekelezwa
ili walioshinda tuzo wafaidi matunda ya tuzo hizo.
“Katika
utekelezaji wa amri zinazotolewa na Mahakama, zipo nyakati ambazo utekelezaji
huo huwa na viashiria vya uvunjifu wa amani kutoka kwa wananchi wasiotaka
utekelezaji huo ufanyike na hivyo Madalali wa Mahakama huitaji msaada wa ulinzi
kutoka jeshi la Polisi”, alisema Jaji Siyani.
Jaji
Kiongozi alisema katika baadhi ya maeneo ya nchi yetu uzoefu unaonesha kuwa
jeshi la polisi limekuwa likisita kutoa ulinzi kwa sababu utekelezaji huo
unahusisha haki ya madai. Alisema kutotoa ulinzi katika hali kama hiyo, husababisha
uvunjifu wa amani au amri za Mahakama kutotekelezwa.
Kwa
upande wa Viongozi wa Serikali, Jaji Kiongozi alisema zipo nyakati ambazo
madalali huzuiliwa kutimiza majukumu yao na viongozi hao wa serikali licha ya
kutambua kuwa kuna amri ya Mahakama inayopaswa kutekelezwa, hutoa amri nyIngine
kinzani au huingia kwenye usuluhishi baina ya pande mbili.
“Tumeshuhudia
kauli mbalimbali zenye kutweza au kudharau maamuzi ya Mahakama lakini bila
kuchukua hatua za kisheria kupinga maamuzi haya. Kauli za aina hiyo zinapotoka
kwa viongozi wa serikali, zinaleta dhana tofauti kabisa na utawala wa sheria”,
alisema.
Alisema
kumekuwa na matukio kadhaa ya viongozi kuishambulia Mahakama kuhusu uadilifu wa
Maafisa Mahakama. Aliongeza kuwa wakuu wa Mikoa na Wilaya wanapofanya hivyo
wakati wao ndio wenyeviti wa kamati za Maadili za Maafisa hawa, inashusha na
kuvunja imani ya wananchi kwa Mahakama.
‘Mahakama
haiwezi kutoa haki kama wananchi hawaiamini na hivyo kuacha kuitumia. Utatuzi
wa migogoro utageukia njia nyingine, na hizo zinaweza kuhatarisha usalama wa
watu na Serikali itajikuta ina kazi kubwa zaidi ya kulinda amani na utulivu katika
nchi” alisisitiza.
Jaji
Kiongozi alisema viongozi wa serikali na hasa wakuu wa mikoa na wilaya ambao
sheria imewapa nafasi za kusimamia maadili ya Maafisa wa Mahakama kwa kuwa ni wenyeviti
wa kamati za wilaya na mkoa, wana wajibu mkubwa wa kusaidia Mahakama kutekeleza
majukumu yake kwa kuijengea imani kwa wananchi.
“Mahakama
inayoaminika ni msingi wa utulivu na amani katika nchi na amani na utulivu ni
mtaji wa maendeleo ambao kila mwananchi anautaka kwa ajili yake na taifa lake”,
alisema Mhe. Siyani.
Katika
hatua nyingine Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imetakiwa
kuelekeza nguvu zake katika usikilizwaji wa mashauri mahakamani ili hatma za
washtakiwa zijulikane mapema na hivyo kuondoa adha ya mashauri hayo kufutwa kwa
kukosa ushahidi na kisha washtakiwa kukamatwa tena na kushtakiwa kwa shauri
lile lile.
Jaji
Kiongozi alisema suala la kuwakamata tena washtakiwa baada ya kufutiwa
mashtaka, au kuyaondoa mashauri na kisha kuyarudisha tena, japo ni utaratibu wa
kisheria lakini unaleta malalamiko na kuifanya Mahakama kuonekana haina nguvu
ya kusimamia amri zake na hivyo kupunguza Imani ya wananchi kwa Mahakama.
Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi wa Magereza Vendeline Raphael Tesha akizungumza wakati wa Mkutano wa Tume na wadau wa utoaji haki mkoani humo. Aliipongeza Mahakama kwa kuongeza kasi ya usikilizwaji wa mashauri iliyosaidia kupunguza msongamano wa Mahabusu na wafungwa katika gereza la Tabora.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni