Jumapili, 25 Juni 2023

VYOMBO VYA UPELELEZI VYATAKIWA KUTUMIA NJIA ZA KISAYANSI KUKUSANYA USHAHIDI

 Na Lydia Churi- Tume ya Utumishi wa Mahakama

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani ametoa rai kwa vyombo vya upelelezi nchini kutumia njia za kisayansi katika kukusanya Ushahidi ili kurahisisha na kuharakisha kazi ya Mahakama ya utoaji wa haki.

Akizungumza na wadau wa utoaji haki katika Mkutano wa Tume mkoani Tabora, Jaji Kiongozi alisema mchakato wa haki jinai utarahisishwa endapo vyombo hivyo vitatumia njia za kisayansi ikiwemo vinasaba (DNA Profiling Tests) mazingira yanaporuhusu na waendesha mashtaka kuwasilisha mahakamani Ushahidi huo.

Alisema kwa zama tulizo nazo hakuna ufanisi bila matumizi ya teknolojia, hivyo alitoa rai kwa vyombo vya upelelezi kwenda sambamba na maendeleo ya karne ya 21 kwa kukusanya ushahidi kisayansi.  

“Matumizi ya ushahidi wa vinasaba sio mageni katika nchi yetu. Wakati mauaji ya albino yaliposhamiri nchini na watuhumiwa kufikishwa mahakani, upande wa mashitaka ulitumia ushahidi wa vinasaba  kuthibitisha makosa pasipo kuacha mashaka yoyote”,alisema. 

Alisema ni matarajio ya Tume na Mahakama kuwa huduma ya utambuzi wa kisayansi wa vielelezo vihusuvyo makosa ya jinai, inayopatikana Dar es Salaam na maeneo mengine machache itapanuliwa na kutolewa katika  kila kanda/Mkoa nchini ili kuharakisha zaidi uchunguzi.

Jaji Kiongozi alisema Tume na Mahakama pia inatarajia kuimarishwa kwa matumizi ya ushahidi wa picha na video katika kuthibitisha makosa ya jinai yaliyowasilishwa mahakamani kwa mujibu wa kifungu cha 36 (1) (2) & (3) cha sheria (the Police Force and Auxiliary Services Act (Cap. 322 R.E 2002) pamoja na Kifungu cha 59 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (the Criminal Procedure Act (Cap 20 RE 2019).

Akizungumzia wajibu wa Serikali katika kuweka mazingira bora ya Mahabusu na wafungwa kutoka Mahakama za Mwanzo, Jaji Siyani alisema ni wakati sahihi kwa Serikali kuanzisha mahabusu kwenye kata zilizo na Mahakama za mwanzo ili Mahakama hizo ziweze kutimiza wajibu wake kwa ufanisi na kurahisisha uhifadhi wa mahabusu na wafungwa.

 Alisema zaidi ya asilimia 70 ya watanzania wanaotafuta haki mahakamani ikiwemo haki jinai, wanahudumiwa na mahakama za mwanzo nchini. Mahakama za mwanzo nyingi ziko mbali na makao makuu ya wilaya ambako kuna uwezekano wa kuwa na gereza la mahabusu na wafungwa.

Kwa mujibu wa kifungu cha 70 cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Wizara ya Mambo ya Ndani, imepewa jukumu la kujenga au kuanzisha Mahabusu kwa ajili ya watuhumiwa na wafungwa wanaohukumiwa na Mahakama za mwanzo kupata hifadhi kabla ya kupelekwa gerezani.

Aidha, sheria imetoa wajibu kwa mamlaka ya Serikali za Mitaa kusimamia mahabusu husika.

“Sote tunafahamu kuwa magereza mengi yalijengwa miaka mingi iliyopita yakikusudiwa kuchukua mahabusu na wafungwa wachache kwa wakati huo. Aidha wilaya nyingi nchini hazina magereza na hivyo kuweka mazingira magumu zaidi ya utekelezaji wa amri za Mahakama za Mwanzo.

Kuhusu umuhimu wa vikao vya Kamati za kusukuma mashauri Kamishna huyo wa Tume alisema kuwa wajumbe wanaounda Kamati hizi wanapaswa kushiriki vikao husika na hivyo kufikia dhamira ya kuanzishwa kwake. Alisema pale inapolazimu kuwakilishwa wahusika wahakikishe wanawapa mamlaka wawakilishi wao na taarifa za mashauri yanayojadiliwa ili kuwawezesha kufanya maamuzi.

Alisema taarifa zilizopo, zinaonyesha kuwa wajumbe wanaotajwa na waraka unaoanzisha kamati hizi za kusukuma mashauri, hawahudhurii vikao husika wao binafsi bali hutuma wawakilishi ambao hawana mamlaka ya kufanya maamuzi na hivyo tija kukosekana.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Mhe. Mustapher Siyani akizungumza na Wadau wa Utoaji Haki mkoani Tabora wakati wa Mkutano wa Tume na wadau hao.
Wadau wa Utoaji Haki mkoani Tabora wakiwa kwenye Mkutano kati yao na Tume ya Utumishi wa Mahakama mkoani humo.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Iringa Mhe. Ilvin Mugeta akitoa Mada wakati wa Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Wadau wa Utoaji Haki mkoani Tabora.

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmilla Sarwat akizungumza wakati wa Mkutano wa Tume ya Utumishi wa Mahakama na Wadau wa Utoaji Haki mkoani Tabora.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni