Jumatatu, 26 Juni 2023

MAHAKAMA MBEYA, MAWAKILI WAKUTANA; JAJI NDUNGURU AWATAKA KUUNGA MKONO MATUMIZI YA TEHAMA

Na Mwinga Mpoli – Mahakama Kuu Mbeya

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Ndunguru amewakumbusha Mawakili wa Kujitegemea kuwa tayari kupokea ujio wa matumizi ya akili bandia na TEHAMA kwa ujumla ili kuunga mkono jitihada za Mahakama zinazolenga kuharakisha huduma ya utoaji haki.

Akizungumza na Mawakili hao hivi karibuni katika kikao cha kujadiliana na kuweka mikakati mbalimbali ili kuboresha uadilifu na kuwepo na kamati ya nidhamu ngazi ya Mkoa kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Mbeya, Mhe. Ndunguru alisema kwamba wote kwa pamoja wawe tayari kupokea mabadiliko hayo na kusisitiza kwamba matumizi ya TEHAMA ni moja ya harakati za mapambano dhidi ya rushwa. 

“Naomba msiwaweke katika wakati mgumu Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama wakati wa mapambano dhidi ya rushwa, bali muwaunge mkono katika harakati za kupambana na rushwa,” alisema Jaji Ndunguru.

Aliongeza kwamba, kwa sasa Mfumo wa Kusajili Kesi unasaidia kuondokana na kuepusha mianya ya rushwa hivyo wasijisahau kwenye suala zima la TEHAMA. “Mawakili kama maafisa wa Mahakama mnapaswa kuwa mstari wa mbele na kushirikiana na maafisa wengine wa Mahakama katika mapambano dhidi ya rushwa” alisisitiza Mhe. Ndunguru.

Alihimiza kuwe na mafunzo ya mara kwa mara na Mawakili wapya ili wapewe taarifa na utaratibu juu ya Kamati ya Nidhamu.

Mawakili hao walishukuru kwa kufanyika kwa kikao hicho na kuahidi kushirikiana na watumishi wa Mahakama katika kuboresha shughuli za Mahakama na kuomba upatikanaji wa vitendea kazi kama kompyuta mpakato kwa kila Wakili ili kuunga mkono mabadiliko ya TEHAMA mahakamani.


Sehemu ya Mawakili wa Kujitegemea waliohudhuria kikao wakimsikiliza Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Ndunguru (hayupo) katika picha. Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Mbeya.
Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Ndunguru akifungua kikao  kilichojumuisha Watumishi wa Mahakama Kanda ya Mbeya na Mawakili wa Kujitegemea waliopo katika Kanda hiyo. 

Sehemu ya Mawakili wa Kujitegemea waliohudhuria kikao wakimsikiliza Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Dunstan Ndunguru (hayupo) katika picha. Kikao hicho kilifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama Kuu Mbeya.

(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni