Jumatatu, 26 Juni 2023

JAJI MKUU ATAKA MABADILIKO KIFIKRA

Na Faustine Kapama-Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewahimiza watumishi wa Mahakama kubadilika kifikra na kuacha kufanya kazi kwa mazoeza ili kwenda sambamba na maboresho ya aina mbalimbali yanayofanyika mahakamani, ikiwemo mfumo mpya wa kielekrioniki wa kuratibu mashauri (e-Case Management).

Mhe. Prof. Juma ametoa rai hiyo leo tarehe 26 Juni, 2023 katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam alipokuwa anafungua mafunzo ya siku mbili kuhusu mfumo huo mpya yanayotolewa kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania.

“Natambua kuhama kutoka mfumo mmoja kwenda mfumo mwingine kunahitaji mabadiliko makubwa ya kifikra. Wakati umefika wa kusisitiza kuwa maboresho yaende sambamba na mabadiliko ya kifikra na fikra ziwe ni za kimaboresho na sio zile za kizamani za kufanya kazi kwa mazoea,” amesema Jaji Mkuu.

Mhe. Prof. Juma amesema mabadiliko na maboresho ya mfumo huo unaifanya Mahakama ya Tanzania kuwa karibu na wananchi na mwananchi wa kawaida atanufaika sio tu kwa kupata taarifa zote muhimu kuhusu kesi yake, bali pia kusogezewa karibu huduma za kimahakama na kurahisishiwa upatikanaji wa haki kwa wakati pasipo kumlazimu kusafiri kufuata ilipo masjala ya Mahakama.

“Maboresho kupitia mfumo huu utaleta mageuzi ya moja kwa moja ya kiuchumi kwa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Mfumo huu wa e-CMS ni hatua muhimu ya Mahakama ya Tanzania katika safari yake ya kuhamia na kuwa Mahakama Mtandao,” amesema.

Jaji Mkuu amesema pia kuwa mfumo huo utafanikisha safari ya Mahakama Mtandao kwa sababu Tanzania tayari inazo Sera na Sheria za kuwezesha kufanikisha matumizi kamilifu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika utoaji wa huduma za Mahakama.

Mhe. Prof. Juma ametaja faida zinazotarajiwa endapo kila mtumishi wa Mahakama ataufahamu mfumo huo na kuwa sehemu ya ufanisi wake.  

“Mfumo huu utaongeza tija, ufanisi na uono wa viwango vya utoaji wa huduma wa kila atakayeutumia, kwa mfano Majaji, Wasajili, Mahakimu, Masjala za Mahakama, wadau wote wa Mahakama na hata kwa wananchi watakaongia katika mfumo kutafuta taarifa,” amesema.

Amesema itafikia wakati hakutakuwa na haja ya kutumia vipimo vya JOPRAS kutathmini utendaji, weledi, uwazi, ufanisi na tija ya watumishi wa Mahakama.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, mfumo huo utaongeza ufanisi katika usimamizi unaofanywa na viongozi wa ngazi mbalimbali wenye majukumu ya kusimamia utekelezaji na usimamizi wa shughuli za utoaji haki.

Alitolea mfano kwa Jaji au Hakimu Mfawidhi ambaye ataongezewa uoni wa kila hatua ambayo shauri lolote linapitia na kufikia mbele ya Jaji au Hakimu bila kuliita jalada au kuomba taarifa ya mashauri kutoka kwa aliye na jalada hilo.

Faida nyingine ni kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za haki jinai na haki madai na kuwezesha taarifa muhimu za mashauri kupatikana kwa yeyote atakayehitaji ambaye ataruhusiwa.

Mhe. Prof. Juma amebainisha kuwa mfumo huo utapunguza gharama zinazohusiano na michakato na hatua mbalimbali ambazo mashauri hupitia na pia utapunguza makosa, kwa mfano kukosewa au kubadilika kwa majina ya wahusika katika kila hatua shauri linapita.

Jaji Mkuu alitumia nafasi hiyo kuwapongeza watumishi wa Mahakama katika Kurugenzi ya TEHAMA na wale wa Idara ya Menejimenti ya Mashauri kwa kujenga mfumo unaoboresha ule wa JSDS2 bila kutegemea wataalamu kutoka nje ya Tanzania.

Amesema mfumo huo umejengwa kwa kuzingatia mahitaji ya Mahakama na kila mshiriki anao wajibu wa kutoa mawazo yanayolenga kuuboresha.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati anafungua mafunzo kuhusu mfumo mpya wa kielektroniki wa kuratibu mashauri. Mafunzo hayo yanahusisha Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania.
Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sylvester Kainda akitoa maelezo ya utangulizi kuhusu mafunzo hayo. 

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani (juu na chini). Wengine waliokaa ni Jaji wa Mahakama hiyo, Mhe. Augustine Mwarija (kushoto) na Mhe. Shaban Lila (kulia).

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani (juu), Msajili wa Mahakama ya Rufani na Naibu Wasajili wa Mahakama hiyo (chini). 

Meza Kuu ikiongozwa na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) ikiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Wakurugenzi na Naibu Wakurugenzi wa Mahakama ya Tanzania.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni