Na Magreth Kinabo-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema mfumo mpya wa kielekrioniki wa kuratibu
mashauri (e-Case Management) utaondoa ucheleweshaji wa usikilizaji wa mashauri,
hivyo kusaidia wananchi kupata haki zao kwa wakati.
Mhe. Prof. Juma ameyasema
hayo leo tarehe 27 Juni, 2023 katika Ukumbi wa mikutano wa Benki Kuu ya
Tanzania jijini Dar es Salaam alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili kuhusu
mfumo huo mpya yaliyokuwa yanatolewa kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani ya
Tanzania.
“Mfumo huu tukiutekeleza
utakuwa na manufaa makubwa ya utoaji haki, kwa kuwa utawezesha shauri
kusikilizwa katika kipindi (kifupi), wananchi kuona haki inavyotolewa,
kupunguza mlundikano wa mashauri mahakamani, kushirikiana na wadau na utaongeza
tija kwenye usimamizi wa mashauri,” amesema Prof. Juma.
Jaji Mkuu ameongeza
kwamba Mahakama inapohama kutoka mfumo wa analojia kwenda kidijitali ni vema taratibu zinazopoteza muda au kuchelewesha katika ushughulikiaji wa mashauri zikaondolewa,
hivyo maeneo ya ucheleweshaji yanatakiwa kuainishwa ili kama sheria
ifanyiwe marekebisho au kanuni zitungwe upya ikiwa ni hatua ya kuendelea
kufanikisha jambo hilo.
“Hii kazi ni endelevu na
sisi tutaendelea kutoa michango yetu ili kuifanya kazi iwe nzuri,”
alisisitiza Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Prof. Juma
amefafanua kuwa hatua inayofanywa katika matumizi ya mfumo huo ni kujenga akili
bandia, hivyo kila mmoja awe sehemu ya kuifundisha mashine hiyo ili iweze
kutumika kwa ubora.
Jaji Mkuu amezipongeza
Kurugenzi za Menejimenti ya Mashauri na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
kwa kuonyesha mabadiliko ya dunia kwa kufanya kazi kwa pamoja. Amesema taaluma
ya sheria bila kushirikiana na taaluma ya TEHAMA haiwezi kufika mbali.
Hata hivyo, Mhe. Prof.
Juma alizishauri kurugenzi hizo kushirikisha watumishi wa masjala kwa kuwa wana
uzoefu utakaosaidia kuendelea kuboresha mfumo huo.
Kwa upande wake, Mwakilishi
wa Majaji waliopata mafunzo hayo, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe.
Ferdinand Wambali, akizungumza baada ya kuhitimishwa mafunzo hayo amesema mfumo
huo utasaidia kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka ambazo zitakuwa
zinapatikana kirahisi na utarahisisha jukumu la utoaji haki kwa wananchi.
“Mahakama imekuwa ikitumia
mfumo wa analojia katika uendeshaji wa mashauri, lakini mfumo unaotarajiwa
kufanya kazi hivi karibuni unalenga kwa sehemu kubwa katika matumizi ya kielektroniki
kuendesha mashauri. Hivyo, tukiutekeleza ipasavyo utaleta manufaa makubwa sana
katika utoaji haki, mashauri yatamalizika kwa haraka na utunzaji wa kumbukumbu
utaimarika zaidi,” amesema.
Sehemu nyingine ya Majaji wa Mahakama ya Rufani (juu mstari wa mbele na mmoja wa kwanza kushoto mstari wa mbele) ikiwa katika mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni