Emmanuel Oguda - Shinyanga
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali, amewataka watumishi wa Kanda hiyo kuzingatia uadilifu, weledi na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi.
Mhe. Jaji Mahimbali ametoa rai hiyo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa kawaida wa Mahakama iliyofanyika tarehe 26 na 27 Juni, 2023 katika Mahakama za Hakimu Mkazi Simiyu, Mahakama za Wilaya Bariadi, Maswa, Meatu, Itilima na Busega.
‘’Huwezi kuwa na weledi pasipo kuwa na uadilifu, halikadhalika huwezi kuwa na uadilifu pasipo uwajibikaji, vyote vinatakiwa kuendana kwa Pamoja,’’ amesema Jaji Mahimbali.
Aidha amewakumbusha watumishi wote wa kanda hiyo kuepukana na vitendo vya rushwa na ukosefu wa maadili ya utumishi wa Umma na Utumishi wa Mahakama kwa kuwa jamii inawategemea katika kutoa haki.
Mhe. Jaji Mahimbali amewasisitiza Mahakimu wote ndani ya kanda ya hiyo kutoahirisha mashauri pasipo sababu za msingi na kuwataka kumaliza mashauri kwa wakati kama ambavyo Mkakati wa umalizwaji mashauri ndani ya kanda unavyotaka. ‘’licha ya kutokuwa na mashauri ya mlundikano, kasi ya usikilizwaji mashauri iongezeke ili kuwe na uwiano baina ya mashauri yanayofunguliwa na yanayomalizwa ili tusiwe na mzigo mkubwa wa mashauri yanayosubiri kusikilizwa ndani ya kanda yetu’’ ameongeza.
Wakati huohuo, Mhe. Jaji Mahimbali amepata fursa ya kutembelea ukarabati mkubwa wa jengo la Mahakama ya Wilaya Maswa linaloendelea kufanyiwa ukarabati ambapo Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya Maswa, Mhe. Enos Misana ametoa taarifa kuwa mkandarasi anatarajia kukabidhi jengo hilo tarehe 31 Julai, 2023.
Pia, Jaji Mahimbali amewasisitiza watumishi wa Mahakama za Wilaya za Itilima na Busega kutunza miundombinu ya majengo hayo pamoja na vitendea kazi vilivyopo kwa kuwa ni ya kisasa na yamejengwa kwa gharama kubwa, hivyo ni matarajio yake kuwa miundombinu hiyo itadumu kwa muda mrefu zaidi.
Katika ziara hiyo, Jaji aliambatana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Warsha Ng’humbu, Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Bi. Mavis Miti, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Mhe. Martha Mahumbuga na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. Gasto Kanyairita.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Frank Mahimbali akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu (hawapo katika picha) wakati wa ziara ya ukaguzi katika Mahakama hiyo.
( Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni