Na Evelina Odemba, Mahakama Morogoro
Wanafunzi wanane kutoka Shule ya Kimataifa ya Morogoro wafanya ziara ya kutembelea Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) kilichopoMorogoro ili kujifunza namna kituo hiko kinavyofanya kazi ya kutoa haki kwa wananchi, na kuaswa kuwa na maadili, nidhamu, heshima, ikiwemo bidii katika masomo yao ili kutimiza ndoto zao za uanasheria.
Wakiwa katika ziara yao ya siku ya kwanza walipata nafasi ya kutembelea ofisi ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe, iliyopo katika jengo la Kituo,hicho ambaye alipata nafasi ya kuzungumza nao na kuwasisitiza mambo mbalimbali.
Mhe. Jaji Ngwembe aliwaeleza wanafunzi hao wenye ndoto ya kuwa wanasheria wa baadae kuwa safari ya kukaa kwenye kiti cha maamuzi ni ndefu, lakini inavutia sana hivyo lazima wawe na bidii katika masomo yao, “ili ukae katika kiti cha maamuzi ni lazima uwe na maadili yasiyokuwa na mashaka, nidhamu isiyokuwa na mashaka, na utendaji kazi usiokuwa na mashaka bila kusahau heshima yako kwenye jamii isiyokuwa na mashaka” alisema.
Aidha katika siku ya pili wanafunzi hao walipata nafasi ya kuudhuria kipindi cha elimu ya sheria katika ukumbi wa Kituo hicho, ambapo kwa siku hiyo elimu ilitolewa na Jaji Mhe. Ngwembe ambaye alizungumzia suala la maadili katika jamii na kugusia umuhimu wa kuwafundisha watoto kusema ukweli hata wanapotoa ushahidi mahakamani, ikiwemo kuwaelezea madhara yaliyowahi kutokea baada ya watoto kufundishwa kutoa ushahidi wa uongo mahakamani.
Wanafunzi wa Shule ya Kimataifa ya Morogoro wanategemea kujifunza kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 12 Juni, 2023 hadi tarehe 16 Juni, 2023 na katika siku hizi watapata nafasi ya kuuzulia vipindi vya elimu vinavyotolewa na Kituo hicho, kusikiliza namna kesi zinavyoendeshwa katika Mahakama ya Wazi, kutembelea ofisi za wadau wa Mahakama zilizopo ndani ya kituoni hapo na kuona namna wanavyoshirikiana na Mahakama katika kutoa haki na mwisho watapata nafasi ya kuelezea namna walivyojifunza.
Tangu kufunguliwa kwa Kituo hicho, licha ya kurahisisha shughuli nzima ya utoaji haki pia kimekuwa kivutio kwa makundi mbalimbali ambayo yamekuwa yakiomba nafasi ya kufika ili kujifunza namna kinavyoendesha huduma zake, ikizingatiwa kuwa vituo vya IJC ni vipya kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla. Mahakama ya Tanzania kwa sasa ina vituo vya IJC sita, ambapo vingine viko Dar es Salaam viwili Temeke na Kinondoni, vikiwemo vya Mwanza, Arusha na Dodoma. Mahakama pia ina mpango wa kujenga vituo vingine tisa katika maeneo kadhaa nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni