Na Magreth Kinabo na Mwanaidi Msekwa
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina ametoa wito kwa Mawakili na Watanzania kuandika vitabu, majarida na mashairi kuhusu Sheria za Kazi na utatuzi wa migogoro ya kazi.
Akizungumza tarehe 14 Juni, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Mahakama hiyo, Mhe. Jaji Mlyambina wakati akipokea vitabu vya ‘Auda’s Index To The Laws Tanzania From 1920 to 2021 Volume 1 hadi 3, ambapo kila volume’ zipo nakala 13, vikiwemo vitabu vingine mbalimbali vya sheria ambavyo jumla yake 218, vilivyotolewa na Wakili na mwandishi wa vitabu vya sheria, Audax. Vedasto. Ambapo amesema Sheria ya Kazi bado ni changa, hivyo watu wanaoandika vitabu vya Sheria ya Kazi na utatuzi wa migogoro ya kazi ni wachache.
Mhe. Dkt. Mlyambina amesema wanataka kuwa na maktaba ya kisasa yenye nakala ngumu za vitabu na laini (kidijitali), hivyo amewataka Watanzania wasikate tamaa ya kuandika vitabu vinavyohusu sekta hiyo.
“ Vitabu ni ‘source of knowledge’( chanzo cha maarifa) na knowledge is power (maarifa ni nguvu) inatokana na maandiko matakatifu wanaosoma Kitabu cha Kitakatifu cha Bibilia Mithali 18 -15 inasema moyo wa mwenye busara hupata maarifa, na sikio la mwenye hekima hutafuta maarifa. Hivyo ukitaka kufanikiwa katika maisha yako yatafute maarifa,” amesema Mhe. Dkt. Mlyambina.
Ameongeza kwamba jamii inaposoma na kuandika vitabu inaacha kumbukumbu ya maandishi, ambapo ni jambo linalowezekana kwa Watanzania. Pia inaimarisha uwezo wa kufikiri.
Mhe. Dkt. Mlyambina amesema kunapokuwa na migogoro ya kazi uchumi wa nchi unadumaa, hivyo ili kutekeleza adhima ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni lazima jamii ikatenga muda vizuri wa kuweza kuokoa watu wanaotaabika na migogoro ya kazi kwa kuandika vitabu vya aina hiyo.
Amefafanua kuwa ili jamii iweze kuandika vitabu inapaswa kujenga afya ya mwili huku akitolea mfano msemo wa Kilatini usemao ‘Mensa. Sana in Corpro Sana’( Akili safi iko kwenye mwili wenye afya). mwili wenye afya njema unakuwa na uwezo wa kutakafari na mawazo mazuri ya kutatua changamoto. Hivyo jamii inatakiwa kuwa na tabia ya kula vyakula vinavyojenga miili na kufanya mazoezi, kwani itawasaidia kuwa na afya safi itakayowawezesha kuandika vitabu.
Kwa upande wake Wakili Msomi Vedasto mwenye uzoefu wa uwakili kwa kipindi cha miaka 20, amesema ametoa vitabu hivyo ili kusaidiana na Mahakama katika shughuli mbalimbali za sheria na kuongeza wasomaji.
Naye Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo alimshukuru Wakili huyo kwa kutoa vitabu hivyo vitakavyosaidia vizuri na kuepukana na makosa ya kutumia sheria zilizopitwa na wakati.
Aidha ameeleza kuwa uandikaji wa vitabu hivyo si kazi rahisi, ni kipaji cha mtu na zawadi pekee iliyotoka kwa Mwenyezi Mungu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina(kushoto) akisalimiana na Wakili na mwandishi wa vitabu vya sheria, Audax. Vedasto aliyefika ofisini kwake kwa ajili ya kukabidhi vitabu mbalimbali vya sheria, ikiwa ni utekelezaji wa ngazo ya tatu ya Mpango Makati wa Mahakama ya Tanzania wa Miaka Mitano( 2021- 2025) ya Kujenga Imani na Wananchi na Kuwashirikisha Wadau katika shughuli za Mahakama.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina(kulia) akizungumza na Wakili Msomi na mwandishi wa vitabu vya sheria, Audax. Vedasto wakati wa makabidhiano ya vitabu mbalimbali vya sheria.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akizungumza na Wakili Msomi na mwandishi wa vitabu vya sheria, Audax. Vedasto aliyefika ofisini kwake kwa ajili ya kukabidhi vitabu mbalimbali vya sheria ( wa kwanza kulia), wengine ni Wakili Pascal Mshanga(katikati kulia) na Wakili Joseph Rugambwa(watatu kulia).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina(wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo(wa kwanza kulia), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga (wa kwanza kushoto).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni