Jumatatu, 12 Juni 2023

MAJAJI SABA WA RUFANI WAPIGWA MSASA; JAJI MKUU AWASIHI KUTOTOFAUTIANA KATIKA MAAMUZI

Na Yusufu Ahmadi, IJA-Lushoto

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Hamis Juma amewataka Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani wasitoe maamuzi yanayokinzana na maamuzi yaliyokwishatolewa na Mahakama hiyo.

Akizungumza leo tarehe 12 Juni, 2023 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto-Tanga wakati akifungua mafunzo Elekezi kwa Majaji saba wakiwemo sita (6) wapya wa Mahakama ya Rufani walioteuliwa hivi karibuni na mmoja ambae hakupatiwa mafunzo hapo awali, Jaji Mkuu amewaasa Majaji hao kutafakari kwa kina maamuzi wanayoyatoa kwa kuwa Katiba ya Tanzania imewapa nafasi ya mwisho ya utoaji wa tafsiri ya haki hapa nchini.

"Huwa tunafanya kazi katika majopo, hivyo jopo moja lisitoe maamuzi ambayo ni tofauti kabisa na majopo mengine, Jaji mmoja wa Rufani akiamua tofauti na ule utaratibu wa kisheria, sisi wengine tunajua amekosea, sasa hiyo inakuwa sio vizuri," amesema Mhe.Prof. Juma.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mafunzo hayo, Jaji Mkuu ameeleza kwamba,  ni vizuri siku zote kutafakari uzito wa maamuzi katika nafasi ya Ujaji wa Mahakama ya Rufani, huku akisisitiza juu ya umuhimu wa kusimamia shauri lolote kuchukua angalau muda mfupi kutafakari, kwa sababu Katiba imewapa Majaji hao nafasi ya mwisho katika kutafsiri haki, hivyo kukitokea makosa yanakuwa ni makubwa na yanachukua muda mrefu kurekebishika.

Kwa upande mwingine, Jaji Mkuu ametoa wito kwa Majaji hao kusoma masuala mbalimbali yanayoendelea duniani yakiwemo ya teknolojia badala ya kusoma tu mambo yanayohusu majalada ya mahakamani, ili wawe na ufahamu mpana utakaowasaidia katika kushughulikia majalada.

Katika mafunzo hayo, Jaji Mkuu ametoa mada kuhusu 'utamaduni wa Mahakama' lengo likiwa ni kuwafanya Majaji hao wapya kutambua taratibu na sheria mbalimbali zinazotumika katika uendeshaji wa mashauri katika Mahakama ya Rufani.

Kwa upande wake Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambae pia ni Mwenyekiti wa jopo la Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija amewaeleza Majaji hao kuwa nafasi waliyopewa waitumie vema kuleta maboresho katika Mahakama ya Rufani.

"Natambua kuwa mlistahili kupata uteuzi huu, sina shaka mtaitumikia kwa uthabiti nafasi hiyo ambayo mmeaminiwa na kupewa, na kama mlikuwa mkiona changamoto yoyote katika Mahakama ya Rufani kwa lengo la kuendeleza maboresho, tambueni sasa ninyi ni sehemu ya kukabiliana na changamoto hizo," amesema Jaji Mwarija.

Naye Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)  ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo amesema kuwa mafunzo Elekezi hayo ni ya tatu kutolewa kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani, ya kwanza yalifanyika mwaka 2019 kwa Majaji nane, ya pili mwaka 2021 kwa Majaji sita na ya tatu ni ya mwaka huu 2023 kwa Majaji saba.

Hafla ya ufunguzi wa Mafunzo hayo imehudhuriwa pia na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor, Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na viongozi mbalimbali wa Mahakama.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifungua Mafunzo Elekezi kwa Majaji saba wa Mahakama ya Rufani wakiwemo sita walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mafunzo hayo ya siku tano yamefunguliwa leo tarehe 12 Juni, 2023 na yanafanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto.
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwezeshaji wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji saba wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija akizungumza jambo wakati wa hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto mkoani Tanga.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani wanaoshiriki katika Mafunzo Elekezi (waliosimama). Wa pili kushoto ni 
Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mwezeshaji wa Mafunzo Elekezi kwa Majaji saba wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija, wa pili kulia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor na wa kwanza kulia ni Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel. 

(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni