Jumatatu, 12 Juni 2023

JAJI MFAWIDHI DAR AKAGUA MIRADI YA UJENZI WA MAHAKAMA WILAYA NA MWANZO

Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Salma Maghimbi amemuagiza Mkandarasi anayejenga majengo ya Mahakama ya Wilaya Ubungo na Mahakama ya Mwanzo Wazo ‘Hill’ jijini Dar es Salaam kuongeza kasi ya ujenzi wa majengo hayo ili kukamilisha ujenzi huo ifikapo tarehe 28 Juni, 2023.

Akizungumza hivi karibuni na Mkandarasi ‘Moladi Tanzania Limited’ alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa Miradi hiyo, Mhe. Maghimbi alisema ni vema kukamilisha kwa wakati ili huduma za Mahakama hizo zianze kutolewa kwa wananchi wa maeneo hayo.

“Naomba muongeze kasi ya ujenzi ili kukamilisha kwa muda tuliokubaliana, kuhusu changamoto zozote ulizonazo nitazifanyia kazi,” alisema Jaji Maghimbi akiwa katika mazungumzo na Mkandarasi.

Akiwasilisha taarifa za Miradi hiyo mbele ya Jaji Mfawidhi, Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Bw. Beatus Mlando, fedha za mradi huu ni mkopo kutoka Benki ya Dunia, kiasi cha shilingi za kitanzania 1.2 Bilioni. 

Kwa mujibu wa Mtendaji huyo, hadi Mei mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 60 na hiyo ni kutokana na kwamba mradi ulisimama kwa miezi minne kuanzia mwezi Oktoba 2022 hadi Februari 2023 kutokana na mashauriano yaliyokuwepo kati ya Mkandarasi na Mshauri wa Mradi kuhusu kufanya ‘variation’ ya kuezeka kwa kutumia chuma ambapo awali mchoro ulikuwa paa lilipaswa kuezekwa kwa mbao.

“Baada ya kufikia muafaka baina ya pande hizo mbili ujenzi ulianza tena Februari, 2023 na Mkandarasi anapaswa kukamilisha na kukabidhi ifikapo tarehe 28/06/2023,” alieleza Bw. Mlando.

Katika hatua nyingine, Jaji Mfawidhi alimuagiza Mtendaji huyo kuwasiliana na Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) ili kuona uwezekano wa kuchonga barabara kubwa ya kuingia kwenye Mahakama kwa kuwa huduma ya utoaji haki ni ya umma hivyo ni muhimu wananchi kuwezeshwa kufika mahakamani.















MATUKIO MBALIMBALI YA UKAGUZI WA MRADI WA UJENZI WA MAHAKAMA YA WILAYA YA UBUNGO



Jaji Mfawidhi Mhe. Salma Magimbi akitia saini kwenye kitabu cha wageni kabla ya kuanza kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la mahakama



Eng. Robert Mabele, Mhandisi anayesimamia ujenzi akitoa maelezo kuhusiana na mradi ikiwa ni pamoja na sababu zilizopelekea mradi kutokamilika katika muda uliopangwa.


Mtendaji wa mahakama Bw. Beatus M. Benedictus akimweleza Jaji Mfawidhi changamoto mbali mbali zinazoukabili mradi wa ujenzi.


Mheshimiwa Jaji Mfawidhi akitoa maelekezo mabali mbali mbali.



Mheshimwa Jaji Mfawidhi akiwa na maafisa wa mahakama alioambatana na nao katika ukaguzi wa mradi wa ujenzi.















Hakuna maoni:

Chapisha Maoni