Jumatatu, 12 Juni 2023

KIKAO KAZI KUANDAA MKAKATI WA MASUALA YA KIJINSIA CHAHITIMISHWA


 

Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe. Victoria Nongwa amehitimisha kikao kazi cha kuandaa Mkakati wa Usawa wa masuala ya Kijinsia wa Mahakama ya Tanzania.

 

Kikao kazi hicho kilichokaa kwa muda wa siku tano katika ukumbi wa Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC), Morogoro ambacho kiliongozwa na Jaji Victoria.

 

Akizungumza wakati wa kufunga kikao kazi hicho, hivi karibuni Mhe. Victoria alitoa shukurani  kwa washiriki wote waliojitoa kuchangia mawazo yao ili kuifanikisha Mahakama katika mkakati wa maboresho hasa upande wa usawa wa kijinsia, hata hivyo aliwaomba washiriki kutoacha  kutoa ushirikiano kwa mambo yatakayohitaji kuboreshwa mara watakapohitajika kufanya hivyo.

 

“Ninawashukuru sana washiriki kutoka taasisi mbalimbali ambao mmeweza kujumuika na sisi na kutoa michango yenu itakayofanikisha mkakati huu, naomba msichoke kutoa mchango wenu tutakapoomba kupata ushirikiano toka kwenu ili kuuboresha,” alisema.

 

Aidha Mhe. Victoria alitoa shukurani kwa uongozi wa juu wa Mahakama ya Tanzania kwa kuwaamini na kuwapa nafasi hiyo adhimu ya kuwa sehemu ya waandaaji wa mkakati huo na kusema kuwa wataendelea kutoa ushirikiano kila watakapohitajika kufanya hivyo.

 

Kikao kazi hicho ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama  ya Tanzania wa Awamu ya Pili 2020/2021 hadi 2024/2025 kupitia Mradi wa Maboresho katika kujenga mazingira bora na rafiki kwa wanawake, watoto na makundi maalum kupata huduma za kimahakama kwa usawa.

 

Mhe. Victoria aliongeza kwamba ili kupata matokeo chanya na andiko la kitaalamu katika kikao hicho Mahakama iliwashirikisha taasisi mbalimbali ikiwemo, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) na Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP).

Mwenyekiti wa kikao kazi, cha Mkakati wa Usawa wa masuala ya Kijinsia wa Mahakama ya Tanzania. ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mbeya Mhe. Victoria Nongwa, (aliyekaa katikati) akiwa katika picha na washiriki wa kikao hicho,(kushoto  kwake) ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmillah Sarwatt,(kulia) ni  Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick .

                                         Sekretarieti    ya kikao kazi .

Wajumbe wa kikao kazi  hicho wakiendelea na kazi.

wajumbe wa Kikao hicho wakifuatilia mada.

Mwenyekiti wa kikao kazi hicho, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mbeya, Mhe. Victoria Nongwa akijadiliana jambo na  Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmillah Sarwatt   (katikati), akiwemo Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania Bi. Beatrice Patrick (kushoto).

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmillah Sarwatt  (kulia) na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Mahakama ya Tanzania Bi. Beatrice Patrick wakifuatilia mada katika kikao kazi hicho.

 


 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni