Jumamosi, 10 Juni 2023

DKT. JULIANA MASSABO JAJI MFAWIDHI MPYA KANDA YA DODOMA

Na Arapha Rusheke na Stanslaus Makendi, Mahakama Kuu Dodoma 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Juliana Massabo amehamishiwa katika Kanda ya Dodoma kuwa Jaji Mfawidhi, kuchukua nafasi kwa mtangulizi wake. Mhe. Gerson Mdemu ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. 

Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mahakama kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Dodoma na kushuhudiwa na wajumbe wa menejiment kutoka Mahakama Kuu, Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za Wilaya Dodoma na Singida. 

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mhe. Mdemu aliainisha mikakati ambayo imefanyika, ikiwemo kuondoa mashauri ya muda mrefu, ambao ni mpango kazi uliopo kufikia mwezi Decemba mwaka huu wa 2023 kutokuwa na mashauri ya aina hiyo katika Kanda ya Dodoma. 

Alisema pia kuwa kumekuwepo na mkakati wa kuimarisha upendo na ushirikiano baina ya watumishi pamoja na wadau wa Mahakama. 

Katika kipindi chote nilichokuwa Dodoma tumeweza kutekeleza Mpango Mkakati wa Mahakama ikiwemo matumizi sahihi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika shughuli zetu tukiwa hapa mahakamani,” alisema Mhe Mdemu. 

Kadhalika, Jaji Mdemu alibainisha baadhi ya changamoto zinazoikabili Kanda ya Dodoma, ikiwemo ufinyu wa bajeti, upungufu wa watumishi na uchakavu wa majengo ya Mahakama, hususani Mahakama za Mwanzo. 

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi mpya ambaye alikuwa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Moshi kwa nafasi hiyo hiyo alimshukuru mtangulizi wake na kuahidi kuwa yote aliyoyaacha atayaendeleza. 

Mhe. Gerson Mdemu ninakushukuru kwa hotuba nzuri ambayo kwangu nadhani ndio itanisaidia sana katika kazi zangu hapa Dodoma. Niwaombe viongozi wenzngu ushirikiano uendelee ili kazi ziendelee kwa wepesi zaidi,” alisema Mhe. Dkt. Massabo.

 

 Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Massabo (kushoto) akipokea nyaraka mbalimbali za ofisi kutoka kwa mtangulizi wake, Mhe. Jaji Gerson Mdemu. Hafla hiyo ya makabidhiano ilifanyika katika Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Dodoma.

Jaji Mfawidhi mpya wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Juliana Massabo akiongea jambo wakati ya hafla hiyo.

 

Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kanda ya Dodoma wakifuatilia tukio hilo la makabidhiano.


Aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na mrithi wake, Mhe. Dkt. Juliana Massabo(kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Fatma Khalfani pamoja na viongozi waandamizi wa Kanda, Naibu Msajili, Mtendaji wa Dodoma na Singida(waliosiamama).
 
Aliyekuwa Jaji Mfawidhi Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na mrithi wake, Mhe. Dkt. Juliana Massabo(kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Fatma Khalfani pamoja na maafisa utumishi na afisa tawala kutoka Dodoma na Singida.

Aliyekuwa Jaji Mfawidhi Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na mrithi wake, Mhe. Dkt. Juliana Massabo(kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Dkt. Fatma Khalfani pamoja na watumishi wa Kanda ya Dodoma.

(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni