Na Stephen Kapiga-Mwanza
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani ametoa wito kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kushirikiana na Mahakama katika kupendekeza namna ambayo inaweza kusaidia kuondoa changamoto zinazojitokeza wakati wa kushughulikia masuala ya mirathi.
Ametoa kauli hiyo leo tarehe 9 Juni 2023, akiwa jijini Dodoma, kwa njia ya video (mtandao) wakati wa akifungua semina ya Majaji, Mahakimu kutoka Kanda ya Ziwa,Mikoa ya Kigoma, Tabora na Manyara , wakiwemo baadhi ya Mameneja wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wa maeneo hayo.
Mhe. Siyani amesema ni umuhimu wa kuimarisha mifumo inayohusu ustawi wa hifadhi ya jamii ambayo inalenga kulinda utu na maisha ya mwanadamu kwa kuendeleza mifumo ya kisheria yenye uwezo kulinda haki za msingi.
“Ili hilo lifanikiwe ni lazima vyombo vyote vya utoaji haki na wadau wote washirikiane.Ni vema kila mmoja wetu akakumbuka kuwa maisha ya mwanadamu hayana thamani bila mifumo ya kisheria yenye uwezo wa kulinda haki za msingi,” anasema Mhe Siyani.
“Suala la Hifadhi ya Jamii linalogusa maisha ya watu, kwa mfano malipo ya mafao yanapohusisha mirathi yamekuwa na changamoto ya mawasiiano kati ya Mahakama na mifuko ya hifadhi ya jamii. Ni muhimu kupitia semina hii kuweza kujadili, kuibua na kupendekeza namna ambavyo utoaji haki katika eneo hili unaweza kurahisishwa na kunufaisha jamii yetu,” anasisitiza.
Mhe Jaji Kiongozi ameongeza kwamba uwepo wa matumizi ya fomu mbalimbali za mirathi ambazo zimekuwa zikitumika kutekeleza amri za Mahakama katika mashauri ya mirathi kwa upande wa Mahakama za Mwanzo ni fomu namba 5 na 6 na Mahakama za Wilaya na Mahakama Kuu ya Tanzania ni matumizi ya fomu namba 80 na 81.
Hivyo uwepo wa fomu hizo umesababisha mifuko ya hifadhi ya jamii kutumia fomu za Mahakama za Mwanzo tu ambazo ni namba 5 na 6 na kushindwa kutumia fomu namba 80 na 81, kwa kuwa kanuni za mifuko hiyo zinatambua matumizi ya fomu namba 5 na 6.
“Ni vizuri basi kupitia semina hii mkajadili changamoto za namna hiyo kwani kwa baadhi ya Kanda zetu za Mahakama Kuu zimelazimika kutumia fomu namba 5 na 6 ambazo kimsingi ziliandaliwa kwa ajili ya matumizi ya Mahakama za Mwanzo zinapotoa amri mbalimbali za utekelezaji wa mirathi,”anasema.
Pia ni vema wakapendekeza mbinu rahisi zaidi za kushughulikia mashauri ya hifadhi ya jamii kwa maslahi ya jamii kwa jumla. Kwani kwa upande wa NSSF peke yake ina jumla ya mashauri 350 ambayo bado yanaendelea katika Mahakama mbalimbali ambayo yamechukua muda mrefu kumalizika na hivvo Mhe. Jaji Kiongozi amewataka Wahe. Majaji na Mahakimu wote kuhakikisha kuwa wanayapa kipaumbele mashauri hayo yanayohusu hifadhi za jamii.
Mhe. Siyani ameongeza kwamba katika kutoa haki kwenye eneo hilo, ni lazima watoa haki pamoja na wadau wajiepushe na kubanwa na mbinu za kiufundi badala yake wajikite kwenye haki zenyewe.
Amefafanua kuwa matumizi ya mbinu za kiufundi katika kufanya maamuzi yamekuwa na athari mbalimbali, ikiwemo kuchelewesha haki lakini pia kuwanyima wananchi wengi haki zao.
Mhe. Siyani amesema ni vema wakapendekeza mbinu rahisi zaidi za kushughulikia mashauri yanayohusu haki na hifadhi za jamii ambazo zitatumika kwa maslahi ya jamii nchini.
“Mbinu hizo ningependa zizingatie usimamizi bora wa mashauri ili kuhakikisha muda unaotumika katika usikilizwaji wa mashauri unafupishwa na hivyo kupunguza gharama kwa wadau,” anasema.
Aidha Jaji Kiongozi amepongeza ushirikiano kati ya Mahakama ya Tanzania na wadau wake hususani Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama utakaokamilika mwaka 2025.
Semina hiyo ya siku mbili imeandaliwa na NSSF kwa kushrikiana na Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT).
Meza kuu ikiongozwa na Rais wa JMAT ikiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa semina hiyo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni