Ijumaa, 9 Juni 2023

SHAURI LA MUDA MREFU KESI YA UGAIDI LAMALIZWA KUSIKILIZWA


Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro imemaliza kusikiliza shauri la ugaidi lililochukua muda mrefu huku likiwa na idadi kubwa ya mashahidi toka pande zote mbili.

Shauri hilo lililoendeshwa kwa njia ya Video (Video Conference) lenye namba 38/2022. lilisikilizwa mbele ya Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro Mhe. Paul Ngwembe ambaye alianza kusikiliza shauri hilo kuanzia tarehe 21 Machi, 2023 na kufikia tamati tarehe 2 Juni, 2023.

Akizungumza ofisini kwake tarehe 8 Jun, 2023 mara baada ya shauri hilo kumalizika Mhe. Ngwembe alisema kuwa ilikuwa ni kesi ngumu iliyohitaji weledi wa hali ya juu ili kutenda haki kwa pande zote mbili. Hasa ikizingatiwa kwamba masuala ya ugaidi ni eneo jipya katika Nchi ya Tanzania.

“Ilikuwa kesi ndefu na ngumu sana ambayo ilikuwa inahitaji weledi mkubwa ili haki iweze kutendeka kwa pande zote mbili. Katika Nchi yetu masuala ya ugaidi ni mageni,jumla ya mashahidi katika shauri hilo walikuwa 55. Upande wa Jamhuri walikuwa  na mashahidi 34 na vielelezo 28, wakati kwa upande wa utetezi walikuwa na mashahidi 21,” alifafanua Jaji Ngwembe.

Jumla ya washtakiwa 21 wanahusishwa na makosa ya ugaidi wa jaribio la mauaji. Makosa hayo yanadaiwa kutendeka katika Wilaya ya Kilombero mwaka 2015. Shauri hili ni miongoni mwa kesi zilizosikilizwa kwa njia ya Mahakama Mtandao (Video Conference) kuanzia mwanzo hadi mwisho. Haya ni maendeleo makubwa kwa kwa Mahakama ya Tanzania yanayotoa picha kuwa huko tunakoelekea Mahakama  ikafikia hatua ya kutotumia karatasi kabisa na bila wahusika wa mashauri hayo kufika mahakamani.

Hata hivyo licha ya kesi hiyo kumalizika bado hukumu yake haijasomwa na kwa mujibu wa Jaji Ngwembe ameeleza kuwa atapanga tarehe ya kusoma hukumu na pia siku watakayosomewa hukumu watapatiwa nakala zao za hukumu.

 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe aliyesikiliza shauri la ugaidi.

   Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro, Mhe. Paul Ngwembe akizungumza ofisini kwake.

Jengo la Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki, ambako shauri la ugaidi lilisikilizwa.

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni