Alhamisi, 8 Juni 2023

JAJI MKUU AWAASA MAJAJI WAPYA SITA WA MAHAKAMA YA RUFANI

Na Magreth Kinabo- Mahakama


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 8 Juni, 2023 amewapokea Majaji sita wapya wa Mahakama ya RufaniTanzania walioteuliwa hivi karibuni baada ya kuripoti ofisini kwake, jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na Majaji hao, Jaji Mkuu, amesema anawapongeza kwa kuteuliwa kwao na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akiwaomba kufanya kazi kwa ushirikiano na bidii katika kuendeleza kazi ya jukumu la utekelezaji wa utoaji haki kwa wananchi.


“Ninawaomba mwuendelee kujisomea mambo mbalimbali ya kidunia ambayo yanatugusa katika kazi za ujaji, yakiwemo masuala yanayohusu mapinduzi ya kiteknolojia,” alisema Jaji Mkuu Prof. Juma.


Majajı hao ni aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia Temeke, Mhe. Zainab  Muruke na aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dar es Salaam, Mhe. Leila Mgonya.


Wengine ni aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Amour Khamis na aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Shule ya Sheria Tanzania, Mhe. Dkt. Benhajj  Masoud.


Kadhalika,  Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, Mhe. Gerson Mdemu na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agnes Mgeyekwa.


Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Jaji Zainab amesema, wanashukuru kwa kuteuliwa kwao na kuahidi kufuata taratibu na maelekezo watakayopatiwa.


Majaji hao waliteuliwa na Rais Samia, tarehe 28 Aprili, 2023 na kuapishwa tarehe 23 Mei, 2023.

    Jaji Mkuu wa Tanznaia, Mhe. Prof. Ibrahim Hamisi Juma akizungumza na Majaji wapya sita wa Mahakama ya Rufani Tanzania.

Jaji wa Muahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Zainab Muruke akisaini kitabnu cha wageni baada ya kufika ofisi ya Jaji Mkuu.

  Majaji wa wapya wa Mahakama ya Rufani Tanzania wakimsikiliza Jaji Mkuu Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati).

  Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wapya sita wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Zainab Muruke (wa tatu kulia), Mhe. Leila Mgonya (wa tatu kushoto), Mhe. Amour Khamis (wa pili kulia), Mhe. Dkt. Benhajj Masoud (wa pili kushoto), Mhe. Gerson Mdemu (wa kwanza kulia), Mhe. Agnes Mgeyekwa (wa kwanza kushoto).

  
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wapya sita wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Zainab Muruke (wa tatu kulia), Mhe. Leila Mgonya (wa tatu kushoto), Mhe. Amour Khamis (wa pili kulia), Mhe. Dkt. Benhajj Masoud (wa pili kushoto), Mhe. Gerson Mdemu (wa kwanza kulia), Mhe. Agnes Mgeyekwa (wa pili kushoto)  na Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania Mhe. Sylvester Kainda (wa kwanza kushoto).

 

 (Picha na Dhillon John- Mahakama)

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni