Na Faustine Kapama na Mwanaidi Msekwa-Mahakama
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni
ya Kazi, Mhe. Dkt Yose Mlyambina amewasihi Mawakili, Walimu wa Vyuo Vikuu,
Wanafunzi na Watanzania kwa ujumla, hasa wale wanaotekeleza sheria kwa namna
mbalimbali, kujenga utamaduni wa kuandika vitabu vinavyotokana na mambo wanayoyaona
kwa vitendo.
Mhe. Dkt. Mlyambina ametoa rai hiyo leo tarehe 6 Juni,
2023 baada ya kupokea vitabu 450 vya rejea vyenye thamani ya zaidi ya millioni
kumi za Kitanzania kutoka kwa Wakili wa Kujitegemea, Msomi Isaack Zake kwa ajili ya Mahakama Kuu
na Mahakama ya Rufani kwenye hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Divisheni hiyo.
“Hatua hii itasaidia Taifa kutotegemea vitabu vya nje
pekee ambavyo vingi viko kinadhalia zaidi na havijibu moja kwa moja changamoto
za mazingira yetu,” alisema katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na Majaji wa
Divisheni hiyo, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo na Mhe. Biswalo Mganga, Naibu Msajili
Mfawidhi, Mhe. Saidi Ding’ohi, Naibu Msajili, Mhe. Cassian Matembele na
watumishi wengine.
Vitabu hivyo ni nakala 150 vyenye jina, “Employers’ Common Mistakes under Labour Laws,”
zingine 150 zenye jina, “How to terminate
an employment agreement” na nakala nyingine 150 zenye jina, “Offences and Penalties under Labour Laws.” Jaji
Mfawidhi amesema vitabu hivyo vitagawiwa kwa Majaji wote wa Mahakama Kuu na
Mahakama ya Rufani.
Mhe. Dkt. Mlyambina amemshurukuru Msomi Zake na
taasisi yake ya Tanzania Labour Guide kwa kuonyesha utayari wa kushirikiana na
Mahakama katika mambo mengi, ikiwemo kutoa elimu ya mahaka pa kazi kuhusu
sheria na pia kutekeleza ahadi aliyoitoa tarehe 3 Mei, 2023 alipokuja
kujitambulisha ofisini kwake.
Alibainisha kuwa Mpango Mkakati wa Mahakama wa Miaka
Mitano (2021-2025) hususani Nguzo ya Tatu inahusu Imani ya Wananchi na
Ushirikishwaji Wadau unaitaka Mahakama kushirikiana na wadau kufanikisha utoaji
wa haki, hivyo vitabu hivyo vina mchango mkubwa katika utekelezaji wa mpango
huo, hasa Nguzo ya Pili ambayo inahimiza upatikanaji wa haki kwa wakati.
Mhe. Dkt. Mlyambina amesema Msomi Zake siyo Wakili wa
kwanza kufanya jambo hilo jema, akikukumbuka mwaka 2021 akiwa Masjala ndogo ya
Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Wakili Audax Kahyendaguza alitoa msaada wa
vitabu mbalimbali alivyoviandika mwenyewe na pia aliwahi kupokea kitabu
kilichoandikwa na Wakili Nguli Ibrahim Bendera na kingine kutoka kwa Wakili na
Mwalimu wa Chuo Kikuu, Dkt. Abdon Rwegasira.
“Niwaombe waendelee kuandika zaidi, kuhamasisha na
wengine kuwa na utamaduni wa kuandika na kushirikiana na Mahakama ya Tanzania
katika kuboresha huduma. Sisi kama Divisheni ya Kazi tupo tayari kuwapa
ushirikiano katika kazi zao za utafiti na uandishi uliotukuka kwa maslahi
mapana ya Taifa letu,” amesema.
Mhe. Dkt. Mlyambina amewasihi watumishi wenzake na Watanzania
kwa ujumla kujenga tabia za kujisomea maandiko mbalimbali, hususani vitabu ili
kuongeza maarifa zaidi ya kukabiliana na changamoto zilizopo.
Jaji Mfawidhi alimnukuu Mwana Falsafa Mzalendo wa
Jamhuri ya Watu wa Uchina ajulikanaye kwa jina la Confucious ambaye aliwahi
kusema, “No matter how busy you may think
you are, you must find time for reading, or surrender yourself to self-chosen
ignorance,” akimaanisha, “Haijalishi umetingwa na majukiumu kiasi gani,
lazima utenge muda wa kujisomea, vinginevyo uchague kuwa mjinga.”
Mhe. Dkt. Mlyambina pia alimnukuu Mwana Falsafa mwingine
Nguli Plato ambaye naye aliwahi kusema, “Books
give a soul to the universe, wings to the mind, flight to the imagination and
life to everything,” akimaanisha, “Vitabu vinaipa nafsi dunia, ni mbawa za
akili, kukurusha kwenye fikra na ni njia ya maisha kwa kila jambo.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Msomi Zake alisema
suala la kukabidhi vitabu hivyo katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi siyo la
kwanza, kwani aliwahi kufanya hivyo mbele ya Jaji Mfawidhi kwa kipindi cha
nyuma, Mhe. Salma Maghimbi kwa nakala chache za kitabu cha “Employers’ Common
Mistakes under Labour Laws.
Wakili huyo ametoa shukrani zake kwa Mhe. Dkt. Mlyambina
na Majaji ambao watakwenda kutumia vitabu hivyo katika shughuli zao. Ameomba kama
wakipata nafasi waandike vitabu au kutoa elimu katika maeneo ambayo wanafanya
kazi, hatua itakayosaidia kukuza taaluma na ufahamu zaidi wa kisheria ambao
Watanzania wanahitaji kuupata.
“Majaji wapo katika nafasi nzuri zaidi ya kutoa
miongozo sahihi kuwezesha wadau kuelewa zaidi na kuepusha migongano ya mara kwa
mara. Nitoe rai kuwa vitabu hivi vinaweza kuwa na mapungufu au maneno ambayo
hayajaangaziwa kwa kina, basi iwe fursa kwenu kukosoa, kuboresha au kuleta
mapendekezo zaidi ya kuibua kazi nyingine nyingi zitakazoweza kuwasaidia vizazi
vyetu kwenye taaluma hii adhimu,” amesema.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (juu na chini) akizungumza baada ya kukabidhiwa vitabu 450 na Wakili Msomi Isaack Zake katika hafla iliyofanyika leo tarehe 6 Juni, 2023.
Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Saidi Ding’ohi akitoa maelezo ya utangulizi katika hafla hiyo.
Wakili Msomi Isaack Zake (kulia) akisisitiza jambo wakati anazungumza kabla ya kukabidhi vitabu hivyo. Kushoto ni Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Saidi Ding’ohi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni