Na Evelina Odemba – Mahakama Morogoro
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Mbeya, Mhe. Victoria Nongwa amesema Mahakama kupitia Mradi wa Maboresho ya huduma zake imedhamiria kusimamia kikamilifu dhima ya utoaji haki sawa kwa wote na kwa wakati kwa kujenga mazingira bora na rafiki kwa wanawake, watoto na makundi maalum.
Mhe. Nongwa ambaye ni Mwenyekiti wa kikao kazi cha kuandaa Mkakati wa usawa wa masuala ya kijinsia kwa Mahakama ya Tanzania aliyasema hayo wakati akifungua kikao hicho jana tarehe 5 Juni, 2023 katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro.
“Mahakama ipo katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wa awamu ya pili 2020/2021 hadi 2024/2025, Mahakama kupitia mradi wa maboresho imedhamiria kujenga mazingira bora na rafiki kwa wanawake, watoto na makundi maalum kwa kupata huduma za kimahakama kwa usawa,” alisema Jaji Nongwa.
Aliwataka wajumbe wa kikao hicho kutoa uzoefu wao ili mawazo yao yawe msaada katika kufanikisha kazi hiyo muhimu ya kutengeneza mkakati wenye lengo la kuongeza wigo sawa kwa wanawake na makundi maalum na katika utoaji haki na utendaji kazi ndani na nje ya Mahakama kwa wananchi wanaohudumiwa na Mhimili huo.
Aidha, aliongeza kuwa baada ya kikao kazi hiko Mahakama inatarajia matokeo chanya ambayo ni kupata uzoefu toka Taasisi nyingine kuhusu namna bora ya kutoa huduma kwa kuzingatia usawa wa wanawake, watoto na makundi maalum pamoja na kuongeza wigo wa Mahakama kushirikiana na wadau wengine katika sekta za umma kuhusu masuala ya kijinsia.
Alisisitiza pia Mahakama itawajengea uwezo wataalamu wake katika usimamizi wa rasilimali kwa kuzingatia usawa wa kijinsia huku akisisitiza washiriki wote kushiriki kikamilifu na kuutumia muda vizuri kutekeleza jambo hilo la kihistoria bila kusahau kuwa mabalozi wazuri katika kuitangaza Mahakama kwa maboresho inayoyafanya.
Awali akisoma taarifa fupi kuhusu kikao kazi hicho, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu-Mahakama ya Tanzania, Bi. Beatrice Patrick alisema kuwa mara baada ya kikao kazi hicho wanatarajia kupata andiko la kitaalamu lenye kuainisha mikakati ya utekelezaji wa masuala ya kijinsia katika mfumo wa utoaji haki na utendaji kazi ndani ya Mahakama ya Tanzania mara baada ya kukamilika.
Naye, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt alisema kuwa ni jambo la kujivunia kwa washiriki wote kwa kuwa wameandika historia katika Muhimili wa Mahakama na Tanzania kwa ujumla.
Kikao hicho cha siku tano kimewakutanisha wajumbe kutoka Taasisi mbalimbali ikiwemo Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu, Wizara ya Katiba na Sheria, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) na Taasisi ya Masuala ya Kijinsia (TGNP).
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania-Kanda ya Mbeya, Mhe. Victoria Nongwa ambaye ni Mwenyekiti wa Kikao Kazi cha kuandaa Mkakati wa usawa wa masuala ya kijinsia kwa Mahakama akifungua kikao kazi hicho jana tarehe 5 Juni, 2023 katika ukumbi wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki (IJC) Morogoro.
Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Desdery Kamugisha pamoja na sehemu ya Wajumbe wa kikao kazi hicho (wawili juu) wakijitambulisha.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni