Na Mwanaidi Msekwa-Mahakama Kazi
Jaji Mfawidhi na Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt Yose Mlyambina hivi
karibuni aliongoza ujumbe wa viongozi wanne waliohudhuria Mkutano wa Baraza Kuu
la Wafanyakazi Dodoma kutoa mrejesho wa kilichozungumzwa na maazimio yaliyofikiwa.
Tukio hilo lilifanyika kama sehemu ya mafunzo kwa
wateja wa ndani ambayo huratibiwa na Kamati ya Elimu Mahakama Kuu Divisheni ya
Kazi. Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi hufanya mafunzo kwa wateja wa nje siku za Jumatatu
na Jumatano na pia mafunzo hufanyika kwa wateja wa ndani siku ya Ijumaa kila
wiki.
Akifungua mafunzo hayo, Mhe. Dkt. Mlyambina aliwataka
watumishi kuwa wasikivu na kumruhusu mwasilishaji, Bw.
Samson Mashalla, aliyekuwa Mtendaji wa Divisheni ya Kazi ambaye amehamishiwa
katika Kituo Jumuishi cha Masuala ya Familia, kueleza kile kilichojiri katika Baraza
Kuu.
Mtendaji huyo aliwapitisha
watumishi kwa ufupi kwenye hotuba ya Mwenyekiti wa Baraza, Jaji Mkuu wa
Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na kuainisha maeneo muhimu
yatakayoboresha ufanisi wa kazi.
Aliendelea
kwa kufafanua umuhimu wa Baraza Kuu la Wafanyakazi na Mabaraza ya Kanda ambapo
Jaji Mkuu aliwataka wafanyakazi washirikishwe kwenye masuala yanayoihusu
Taasisi wanayoifanyia kazi.
Aliwasilisha
pongezi kutoka kwa Jaji Mkuu kwa wafanyakazi kwa kuwa wao ndiyo msingi wa mafanikio
ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama na Programu za Maboresho.
Kutokana na hotuba ya Jaji Mkuu kuelezea umuhimu wa Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bw. Mashalla aliwahimiza
watumishi kuwa mfano wa kuigwa na Taasisi zingine katika matumizi ya teknolojia
kutoa huduma kwa umma.
Kuhusu maslahi ya wafanyakazi, alieleza kuwa Tume ya
Utumishi wa Mahakama imewasilisha kwa Rais mapendekezo ya viwango vya
mishahara, posho na stahiki zingine. Mtendaji huyo alieleza kuwa kuanzia mwaka
ujao wa fedha inatarajiwa takribani watumishi wote watapewa posho ya mavazi kwa
viwango tofauti kulingana na kada zao.
Bw. Mashalla pia aliainisha sifa za mtumishi wa Mahakama karne ya 21 kutokana na hotuba ya Jaji Mkuu kuwa lazima kuzingatia lengo la nne la Dira ya Maendeleo ya Taifa, ambalo linahimiza uwepo wa jamii iliyoelimika vema na inayojifunza.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina akizungumza wakati
akifungua mafunzo ya Mrejesho wa Mkutano wa Baraza Kuu la Wafanyakazi.
Mtendaji wa Mahakama ambaye amehamishiwa katika Kituo
Jumuishi cha Masuala ya Familia, Bw. Samson Mashalla akitoa mada kwa viongozi
na watumishi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Naibu Msajili Mfawidhi Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Saidi Ding’ohi akichangia mada.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (wa pili kushoto), Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Biswalo Mganga (wa pili kulia) na watumishi wengine wakifuatilia uwasilishaji wa taarifa ya Baraza Kuu.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Yose Mlyambina (katikati) akiwa katika picha ya pamoja naviongozi waandamizi na watumishi wengine wa Mahakama hiyo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni