Na Dillon John-Divisheni ya Ardhi
Jaji Mfawidhi mpya wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Elinaza Luvanda amekabidhiwa
rasmi ofisi na mtangulizi wake, Mhe. Agnes Mgeyekwa ambaye amekuwa Jaji wa
Mahakama ya Rufani.
Hafla ya makabidhiano
hayo ilifanyika hivi karibuni katika Chemba ya Jaji Mfawidhi na kushuhudiwa na wajumbe
wa Menejimenti wa Divisheni hiyo Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba
ya Menejimenti, Mtendaji wa Mahahakama katika Divisheni ya Ardhi, Bw. Anatory
Kagaruki alieleza kuwa watumishi wanaishi kama familiÄ… moja na Majaji na
wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kikamilifu, ikiwemo kushiriki katika vikao
kazi mbalimbali pamoja na wadau ili kuimarisha huduma za utoaji haki kwa
wananchi.
Alitaja moja ya vikao
kazi hivyo ni kikao kikubwa cha wadau kilichofanyika katika Ukumbi wa Kambarage
Benki Kuu ya Tanzania. Alisema kikao hicho kilifunguliwa na Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali.
“Kuna mafanikio mengi
yamepatikana ambayo yalikuwa yanasimamiwa na Mhe. Mgeyekwa. Amekuwa kiongozi
mzuri na mama mlezi wetu kwa nafasi yake aliyokuwa nayo,” alisema.
Akizungumza wakati wa
makabidhiano hayo, Mhe. Mgeyekwa aliainisha mafanikio yaliyopatikana katika
Divisheni hiyo, ikiwemo kuondoa mlundikano wa mashauri, kujenga ushirikiano
imara kwa watumishi, wadau na kuleta upendo na ushirikiano baina yao wote.
“Katika kipindi chote
tumeweza kuelekeza fedha katika usikilizaji wa mashauri na kwa matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa asilimia 100,” alisema Mhe. Mgeyekwa.
Naye Jaji Luvanda alishukuru
kwa mapokezi mazuri kutoka kwa mtangulizi wake, huku akieleza kuwa yote aliyotekeleza
atayazidisha na kufanya Divisheni hiyo iendelee kufanya vizuri zaidi ya hapo.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni