Na Mary Gwera, Mahakama
Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amemwakilisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika hafla ya mapokezi ya ndege mpya ya mizigo aina ya Boeing 676 – 300F.
Mtendaji Mkuu huyo pamoja na Viongozi wengine wa Serikali na wageni wengine waliungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipokea ndege hiyo jana tarehe 3 Juni, 2023 katika Viwanja vya Ndege vya Kimataifa vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Dkt. Samia, aliwaomba watanzania kuendelea kuwaombea mema viongozi wa Serikali ili wapate nguvu ya kufanya maendeleo ya nchi na kuendelea kuwa pamoja na Serikali katika kufanya shughuli za maendeleo.
“Naomba muendelee kuwa pamoja nasi, tuombeeni tupate nguvu, tufanye kazi tupate mapato, tumeombwa ndege nyingine ya mizigo tunalifanyia kazi” amesema Rais Mhe. Dkt. Samia.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa, amesema kuwa Wizara ya ujenzi inatambua Serikali imekuwa ikitoa kipaumbele katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mhe. Prof. Mbarawa amesema kuwa ujio wa ndege ya mizigo unakwenda kuwa chachu kwa wafanyabiashara wa wanatanzia na nchi mbalimbali.
“Wizara ya ujenzi itaendelea kuiboresha miundombinu ya viwanja mbalimbali vya ndege ili kuwezesha mashirika ya ndege ndani na nje kwa kutoa huduma kwa ufanisi zaidi” alieleza Prof. Mbarawa.
Akizungumza katika mahojiano maalum na Mwandishi wa Habari hii, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Prof. Elisante Ole Gabriel amepongeza jitihada ambazo Mhe. Dkt. Samia anafanya katika eneo la usafirishaji na maeneo mengine yote yakilenga kuleta maendeleo ya nchi.
“Uwepo wa ndege hii ambayo inabeba takribani mizigo yenye uzito wa tani 54 kwa kiasi kikubwa utachachua uchumi wetu, na uchumi wa nchi unapokua unasaidia pia kuboresha miundombinu ya utoaji haki nchini,” alisema Prof. Ole Gabriel.
Ameongeza kwamba, uchumi wa wananchi unapokua migogoro ya kijamii pia inapungua na usuluhishi pia unakuwa mrahisi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi, amesema kuwa Kampuni ya Ndege ya ATCL katika kutekeleza mpango wake wa pili wa miaka mitano kwa mwaka wa fedha 2022/ 2023 hadi 2026/2027 inatakiwa kuwa na ndege 20 ikiwemo ndege za masafa mafupi nane (8).
“Mapokezi ya ndege hii inaifanya ATCL kuwa na ndege 13 zilizopo, ndege tatu zinaendelea kuundwa, ndege mbili zinatarajiwa kuwasili nchini mwaka huu na nyingine mwaka 2024” amesema Matindi.
Mhandisi Matindi amesema kuwa ujio wa ndege ya mizigo inaiwezesha ATCL na kuifanya Tanzania kupata fursa ya kusafirisha mizigo kwenda nchi mbalimbali. Mizigo hiyo ni minofu ya samaki kutoka kanda ya ziwa, dagaa kutoka na samaki wa mapambo kutoka ziwa Victoria, nyama kutoka mikoa ya Kanda ya ziwa, Kaskazini pamoja na katikati ya nchi.
Mizigo mingine ni maua, matunda na mboga mboga kutoka Mikoa ya Kaskazini mwa nchi pamoja na mazao ya baharini kutoka Zanzibar na maeneo mengine kutoka ukanda wa bahari ya Hindi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na meza kuu wakimpokea Rubani Kiongozi wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) Neema Swai (kushoto) baada ya kuwasili kutoka nchini Marekani katika viwanja vya ndege vya Kimataifa vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere jana tarehe 3 Juni, 2023. Wa pili kulia ni Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel aliyemwakilisha Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni