Na Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro
Maandalizi ya Mkutano wa
Mwaka wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania unaotarajiwa kuanza kesho tarehe 27
Julai, 2023 mjini hapa chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma, yamekamilika.
Msajili wa Mahakama ya
Rufani, Mhe. Sylvester Kainda amesema kuwa tayari Viongozi Wakuu wa Mahakama,
Majaji wa Mahakama ya Rufani na wajumbe wengine wameshaanza na wanaendelea kuwasili.
“Maandalizi ya Mkutano
wetu yameshakamilika. Tayari tumeshampokea Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma, Majaji wa Mahakama ya Rufani na wajumbe wengine wameshaanza
kuwasili kwenye eneo la Mkutano,” amesema.
Amemtaja Kiongozi
mwingine ambaye ameshawasili katika eneo la Mkutano utakaofanyika katika Hoteli
ya Nashera mjini hapa kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Mustapher Mohamed Siyani, ambaye ni miongoni mwa Viongozi wa Mahakama ya
Tanzania ambao wamealikwa kwenye Mkutano huo.
Viongozi wengine waalikwa
ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili
Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na Msajili wa Mahakama Kuu, Mhe.
Sharmillah Sarwatt.
Wajumbe wengine wa
Mkutano huo ni Naibu Wasajili wa Mahakama ya Rufani, baadhi ya Wakuu wa Idara na
watumishi wa Mahakama ya Rufani ambao nao wameshawasili.
Kwa mujibu wa ratiba
iliyotolewa leo tarehe 26 Julai, 2023, taarifa na mada mbalimbali
zitawasilishwa katika Mkutano huo wa siku mbili unaotarajiwa kumalizika tarehe
28 Julai, 2023. Katika siku ya kwanza, taarifa kadhaa zitawasilishwa, ikiwemo
inayohusu mashauri kwa kipindi cha Januari-Disemba, 2022.
Miongoni mwa taarifa
zitakazowasilishwa siku ya pili ya Mkutano ni ile inayohusu hatua iliyofikiwa ya
Mpango Mkakati wa Mahakama na hatua ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi wa
maboresho na kupata taarifa ya hali ya mifumo ya Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano (TEHAMA), maboresho yanayoendelea na safari ya kuelekea Mahakama
mtandao.
Pia kutakuwepo na
uwasilishaji wa mada mbalimbali kutoka kwa wawezeshaji wabobezi, wakiwemo Majaji
wa Mahakama ya Rufani wastaafu, Mhe. Edward Rutakangwa na Mhe January Msoffe.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Mwanaisha Kwariko akipandisha ngazi baada ya akiwasili katika Hoteli ya Nashera mjini Morogoro.
Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Winfrida Korosso akiwasili katika Hoteli ya Nashera mjini Morogoro.
Vijana wapo kazini kuweka mambo sawa.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni