Na Francisca Swai – Mahakama Musoma.
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma hivi karibuni imefanya kikao kazi kilichojumuisha watumishi wa Mahakama Kuu Musoma, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Mahakama za Wilaya na Mwanzo Musoma na Butiama pamoja na wadau kutoka sekta ya Afya, Mfuko wa Pensheni kwa watumishi wa umma (PSSSF), Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Akifungua kikao kazi hicho Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Mhe. Fahamu Mtulya aliwaasa watumishi kuwa watulivu na wasikivu ili waweze kufaidika na kikao kazi hicho kilichohusisha wataalamu mbalimbali watakaowasilisha mada muhimu zitakazo wasaidia katika utendaji kazi wao wa kila siku na aliwashukuru wadau kwa kukubali mwaliko wa kuhudhuria kikao kazi hicho kwa ajili ya kuwaelimisha watumishi juu ya masuala mbalimbali muhimu.
“Kikao hiki ni kina lengo la kutekeleza maelekezo yaliyotolewa kwenye mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mahakama ya Tanzania lililofanyika Jijini Dodoma tarehe 18 – 19 Mei, 2023 pamoja na maombi ya watumishi ya kukutana pamoja, kufahamiana, kujadili mambo mbalimbali ya kikazi na kijamii,” asema Mhe. Jaji Mtulya.
Akizungumza na watumishi hao, Afisa Mafao Mwandamizi Bw. Nuru Mahinya kutoka Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) alieleza mabadiliko ya sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii yaliyotokea mwaka 2018 yalisababisha kuanzishwa kwa mfuko wa PSSSF, shughuli zinazofanywa na mfuko ikiwa ni pamoja na ulipaji wa pensheni kwa watumishi wa umma, wajibu wa mwajiri na mtumishi kwa mfuko huo.
Mahinya aliwaasa watumishi wa umma kufuatilia michango yao mara kwa mara wakati bado wako katika utumishi kwa kuwa inasaidia kufanya marekebisho kwa wakati tofauti na pale ambapo mtumishi ameshastaafu. Pia alisisitiza watumishi wa umma kujiandaa kustaafu mapema ili kuondoa changamoto kubwa zinazotokea baada ya kustaafu bila maandalizi ya kutosha.
Naye Afisa Udhibiti Ubora Dkt. Simeon Maziku pamoja na Afisa Uanachama Mwandamizi Bi. Felister Renatus kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NIHF) walielezea lengo la mfuko huo ambalo ni kuratibu matibabu kwa watumishi wa umma na wananchi wote. Walieleza pia kuwa katika uchangiaji mtumishi wa umma anachangia asilimia 3 ya mshahara wake na mwajiri wake pia anawasilisha asilimia 3 katika mfuko huo kila mwezi. Aidha, walieleza kuwa mfuko huo una zaidi ya vifurushi 60 ambavyo mtumishi pamoja na mwananchi wanaweza kufaidika navyo.
Kwa upande wa Afya Mratibu wa Huduma za Afya ya Kinywa na Meno, Dkt. Ndalahwa Kamari pamoja Mratibu wa magonjwa yasiyoambukiza Mkoa wa Mara Bi. Esther Muya walielezea mambo mbalimbali ya afya ikiwemo umuhimu wa kupima mara kwa mara ili kuzijua afya zetu jambo litakalosaidia kudhibiti magonjwa yanayoingia mwilini katika hatua zake za awali.
Wataalamu hao wa afya walieleza pia kuwa magonjwa yasiyoambukiza kwa sasa ni mengi na hatari kwani ndio yanayoongoza kwa asilimia 75 kusababisha vifo vya watu wengi.
“Sababu kubwa zinazosababisha magonjwa hayo ni mtindo wa Maisha, ikiwemo matumizi makubwa ya bidhaa za viwandani, ugonjwa wa kisukari, matumizi ya dawa za presha, msongo wa mawazo ambao huathiri afya ya mwili hivyo kusababisha magonjwa,” walisema wataalamu hao.
Wataalamu hao walisisitiza ufanyaji wa mazoezi mara kwa mara, kuacha matumizi ya pombe, kupunguza kukaa kwa muda mrefu, kulala usingizi wa kutosha na kuzingatia lishe bora ili kuimarisha afya ya mwili.
Naye Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa Bw. Anthony Gang’oro alieleza kuhusiana na rushwa na sababu kubwa ya rushwa ni umasikini na mmomonyoko wa maadili. Pia aliwaasa watumishi kufanya kazi zao kwa kuzingatia sheria, kutopokea hongo, kutotumia vibaya ofisi na madaraka, kutoa dhamana kadri ya taratibu, kutenda haki katika kufanya maamuzi pamoja na kuridhika na vipato halali. Kwa kuwa kufanya hivyo kutasaidia kujenga jamii yenye maadili na kupunguza uhalifu.
Aidha, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Moshi alipata nafasi ya kuuelezea Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2020/2021 – 2024/2025. kwa kuonesha namna ambavyo Kanda ya Musoma ilivyofanikiwa kuutekeleza hasa katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA), usikilizwaji wa mashuri kwa wakati, uanzishwaji wa mahakama mpya, ushirikiano na wadau pamoja na ukarabati wa Mahakama za Mwanzo.
Naye Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Bw. Festo Chonya aliwapongeza watumishi hao, kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika mwaka wa fedha 2022/2023 ulioleta mafanikio makubwa kwenye Kanda hiyo. Pia aliwataka watumishi hao, kuendelea kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo mbalimbali katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku na kuwapongeza watumishi kwa utulivu na usikivu muda wote wa kikao kazi hicho.
Katika kikao kazi hicho watumishi walipata wasaa wa kuuliza maswali mbalimbali, kupata ufafanuzi wa masuala yaliyokuwa yakiwatatiza, kupata taarifa ya mfuko wa maafa wa watumishi Kanda ya Musoma na masuala mengine mengi ambayo waliyafurahia.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma Bw. Festo Chonya akiongea na watumishi (hawako pichani) waliohudhuria kakao kazi cha watumishi wa Kanda hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma hivi karibuni.
Mlinzi wa Mahakama ya Mwanzo Bunda Mjini, Bw. Julius Magese akiuliza swali kwa mwezeshaji kutoka Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF).
Jaji wa Mahakama Kuu Musoma, Mhe. Marlin Komba akisalimia watumishi pamoja na kuwasisitiza kuzingatia yale waliyoelekezwa katika kikao kazi.
Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Moshi akiwasilisha mada ya Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania na jinsi unavyotekelezwa katika Kanda ya Musoma kwa watumishi hao.
(Habari hii imehaririwa na Magreth Kinabo- Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni