Alhamisi, 27 Julai 2023

MAFANIKIO MAKUBWA YAPATIKANA MAHAKAMA YA RUFANI IKITEKELEZA WAJIBU WA KIKATIBA

·Jaji Mkuu afungua Mkutano wa Mwaka Mahakama ya Rufani

·Atahadhalisha mafuriko ya mashauri kutoka Taasisi Haki Jinai

Na Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo tarehe 27 Julai, 2023 amefungua Mkutano wa Mwaka wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania na kuwapongeza Majaji wote na watumishi wengine wa Mahakama hiyo kwa kutimiza wajibu wao Kikatiba kuhusu utoaji haki kwa mafanikio makubwa.

Akizungumza na Majaji, wajumbe na wageni wengine waalikwa katika siku ya kwanza ya Mkutano huo wa siku mbili unaofanyika katika Hoteli ya Nashera mjini hapa, Mhe. Prof. Juma ameeleza kuwa Majaji wanatekeleza wajibu wao kwa weledi na ufanisi mkubwa kupitia vikao vyao vya Mahakama ya Rufani.

“Pongezi zangu kwa Majaji wa Rufani haziwaachi watumishi wengine wote walioisaidia Mahakama ya Rufani kutekeleza wajibu wake. Kwa mujibu wa taarifa ya Msajili Mkuu ya mwaka 2022, Mahakama ya Rufani ilimaliza jumla ya mashauri 1,890 ambayo ni mengi zaidi ya yale yaliyomalizika mwaka 2021 ambayo ni mashauri 1,879. Taarifa hizi zinaonesha kuwa haturudi nyuma, hivyo tunastahili pongezi kwa jitihada za kila mmoja katika kufikia mafanikio haya,” amesema.

Jaji Mkuu alitumia nafasi hiyo kuwasihi watumishi wa Mahakama kujiwekea utamaduni wa kufuatilia kwa ukaribu mabadiliko yanayotokea nje ya Mahakama, ikiwemo matumizi ya teknolojia za kisasa, hususan “Artificial Intelligence,” na kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa hivi karibuni na Ripoti ya Tume ya kuangalia jinsi ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai nchini.

Amesema kuwa Mahakama ya Tanzania ni miongoni mwa Taasisi zilizoangaliwa na Tume hiyo ambayo imetoa mapendekezo yake kuhusiana na masuala iliyobaini na yanayohitaji maboresho, ikiwemo mashauri kuchukua muda mrefu mahakamani bila kusikilizwa.

“Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mkuu Mstaafu, Mhe. Mohamed Chande Othman, wananchi wanalalamikia sana kuhusu mashauri yaliyokwama kwa muda mrefu katika Mahakama zetu bila kusikilizwa. Tafadhali someni ripoti hiyo ili kwa pamoja tuje na mawazo ya kukabiliana na changamoto hiyo pamoja na changamoto zingine zinazoipunguzia sifa Mahakama kwa ujumla,” amesema.

Mhe. Prof. Juma amebainisha pia kuwa Tume ya Kuboresha Taasisi za Haki Jinai imeainisha maeneo ambayo wananchi wameagiza Taasisi zote katika mfumo wa Haki Jinai yaboreshwe na kubadilishwa, jambo ambalo Mahakama ya Tanzania itaguswa na kuhusika na maboresho yatakayofanyika katika Taasisi zingine za Haki Jinai.

Alitolea mfano wa eneo lililoguswa linalohusu hatima ya matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambapo Tume ilibaini kuwa Taasisi za Haki Jinai zinakabiliwa na changamoto ya mifumo kutosomana.

Jaji Mkuu amesema Mahakama ya Tanzania haiwezi kuyakwepa mapendekezo ya Tume hiyo ya uwepo mfumo jumuishi wa haki jinai unaosomana utakaounganisha Taasisi za Haki Jinai utakaosaidia katika kubadilishana taarifa.

“Hivyo basi, mfumo mpya wa Mahakama wa Usimamizi wa Mshauri (e-Case Management System) ni lazima ujitayarishe kuunganika, kusomana na kubadilishana taarifa na mfumo tarajiwa wa Taasisi za Haki Jinai nchini,” amesema.

Katika Mkutano huo, Jaji Mkuu pia aliwataka watumishi wa Mahakama kujitayarisha na mafuriko ya mashauri yatakayokana na upelelezi bora kutoka Taasisi za Haki Jinai kwa kuzingatia mapendekezo ya Tume katika upelelezi na ukusanyaji wa ushahidi wa kisayansi na kwa kuzingatia maendeleo makubwa ya teknolojia.

Mhe. Prof. Juma amesema kuwa Mahakama haitaeleweka kwa jamii itakaposhindwa kupokea na kutumia ushahidi wa kisayansi utakaozalishwa na mifumo bora ya kiupelelezi itakayojengwa.

Ameeleza kuwa maboresho ndani ya taasisi za upelelezi na uchunguzi kutoka katika taasisi mbalimbali za upelelezi wa makosa ya jinai na kuanzisha mamlaka mpya na huru ya upelelezi inayojitegemea yatahitaji mabadiliko na maboresho makubwa katika ngazi zote za Mahakama.

“Mahakama isipojitayarisha kubadilika kulingana na maboresho katika Taasisi za Haki Jinai, mapungufu yetu Mahakama yataonekana wazi na tutanyooshewa vidole vya lawama na wananchi na Mihimili mingine ya Dola,” amesema.

Viongozi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania wamealikwa katika Mkutano huo. Miongoni mwa viongozi hao ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah Sarwatt.

Wengine ni Majaji wa Mahakama ya Rufani Wastaafu, Mhe. January Msoffe na Mhe. Edward Rutakangwa, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali ndani ya Mahakama ya Tanzania.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (juu na chini) akieleza jambo alipokuwa anafungua Mkutano wa Mwaka wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania mjini Morogoro leo tarehe 27 Julai, 2023.

Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani (juu na chini) ikimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha). 

Sehemu nyingine ya Majaji wa Mahakama ya Rufani (juu na chini) ikimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha). 

Sehemu ya Majaji wa Mahakama ya Rufani (juu) ikimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (hayupo katika picha). Chini ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (wa kwanza kushoto) na Majaji wengine wa Mahakama Kuu.

Sehemu ya Viongozi Waandamizi wa Mahakama ya Tanzania (juu na chini) wakiwa katika Mkutano huo. 

Sehemu yingine ya Viongozi na Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa katika Mkutano huo. 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni