Alhamisi, 27 Julai 2023

MAHAKAMA SONGWE YAZINDUA VILABU VYA ELIMU KATIKA SHULE ZA SEKONDARI

Na Mohamed Kimungu, Mahakama-Songwe

Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe imezindua vilabu ‘clubs’ mbili katika shule za Sekondari za Mkoani Songwe ambazo ni Shule ya Sekondari Ilolo iliyopo Wilaya ya Mbozi na Shule ya Sekondari Maweni lengo likiwa ni kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusiana na masuala mbalimbali ya sheria na maboresho yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania.

Akizungumza hivi karibuni alipotembelea Shule hizo, Hakimu Mkazi Mwandamizi na Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu Mkoa wa Songwe, Mhe. Vitalis Changwe ameeleza kwamba, dhumuni la kuanzishwa kwa vilabu hivyo ni kuendelea kuelimisha umma wakiwemo wanafunzi ili kupenda kujihabarisha na kuwa na ufahamu wa masuala  mbalimbali ya sheria lakini pia kufahamu majukumu ya Mahakama na jitihada inazofanya katika kuboresha huduma ya utoaji haki nchini.

“Mbali na kutoa elimu kwa wanafunzi, Mahakama pia itatoa elimu kuhusiana na masuala mbalimbali ya sheria na kuhusu Mpango Mkakati na vilevile kuwahamasisha wanafunzi kuipenda na kujielekeza katika fani ya Sheria,” alisema Mhe. Changwe.

 Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari Ilolo, Bw. Paul Mahenge amefurahishwa na uamuzi wa Mahakama kuanzisha vilabu ‘clubs’ katika shule huku akisema kuwa uamuzi huo utasaidia wanafunzi kufahamu masuala mbalimbali ya kisheria kupitia vilabu ‘clubs’ hizo na hivyo kujiepusha na uvunjaji wa Sheria za nchi lakini kujua namna sahihi ya kutafuta haki zao katika Mahakama ya Tanzania. 

Bw. Mahenge aliongeza kuwa, wanafunzi wataongeza uelewa kama ambavyo clubs za taasisi nyingine zimekuwa zikifanya kama vile Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na nyingine.

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe, Mhe. Hassan Makube amebainisha kuwa, atahakikisha kuwa vilabu hivyo vinakuwa hai na wanafunzi watapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Mahakama mkoani Songwe kwa lengo la kujifunza. Hali kadhalika, aliongeza kwa kueleza kuwa Uongozi wa Mahakama Mkoa wa Songwe utakuwa unavitembelea vilabu hivyo mara moja kila mwezi na kutoa mafunzo.

Kwa upande wa Shule ya Sekondari Ilolo iliyopo Wilaya ya Mbozi jumla ya wanafunzi 113 wamejiunga na Klabu hiyo na kwa upande wa Shule ya Sekondari Maweni iliyopo Wilaya ya Songwe jumla ya wanafunzi 200 wamejiunga.


Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ilolo wakimsikiliza kwa makini Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya Mbozi na Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu Mkoa wa Songwe, Mhe. Deusdedith Changwe.

Hakimu Mkazi Mwandamizi Mahakama ya Wilaya Mbozi na Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu Mkoa wa Songwe, Mhe. Deusdedith Changwe akizungumza jambo na wanafunzi.


Hakimu Mkazi Mahakama ya Mwanzo Mlowo, Mhe. Tagha Komba  akifafanua jambo mbele ya wanafunzi (hawapo katika picha).

Picha ya watumishi wa Mahakama Songwe, Walimu pamoja na wanafunzi.

(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni