Na Francisca Swai – Mahakama Musoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Musoma, Mhe. Fahamu Mtulya amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Said Mtanda huku akisema kuwa, ni muhimu viongozi kukutana kwa ajili ya kufahamiana na kujenga ushirikiano mzuri katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kulijenga Taifa.
Katika mazungumzo baina yake na Mhe. Mtanda yaliyofanyika tarehe 25 Julai, 2023 alipomtembelea Mkuu huyo wa Mkoa, Mhe. Mtulya alisema ni muhimu kushirikiana ili utendaji kazi uende vizuri lakini pia aliekeleza kuhusu nguzo ya tatu ya Mpango Mkakati wa Mahakama unaohusu ushirikiano na wadau jambo ambalo pia limekuwa likisisitizwa na viongozi wa juu wa Mahakama ikiwemo Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Ibrahim Juma.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Said Mtanda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili kwa Maafisa wa Mahakama ngazi ya Wilaya na Mkoa, alishukuru kwa jambo hilo jema la kufahamiana na kusema kuwa mahusiano mazuri yatasaidia viongozi hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, kutatua kero za wananchi kwa pamoja ili kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati.
Katika ziara hiyo fupi, Jaji Mfawidhi aliongozana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Mhe. Frank Moshi, Mtendaji wa Mahakama Kuu Musoma, Bw. Festo Chonya, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma, Mhe. Erick Marley na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Musoma, Mhe. Aristida Tarimo.
Viongozi wa Mahakama Kanda ya Musoma wakifurahi kwa pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Said Mohamed Mtanda walipomtembelea ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha na kufahamiana.
(Taarifa hii imehaririwa na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni