·Bado asilimia saba tu kufikia 100 umalizaji mashauri
Na
Faustine Kapama-Mahakama, Morogoro
Kasi ya kumalizika kwa
mashauri (clearance rate) katika Mahakama ya Rufani ya Tanzania imepanda kutoka
asilimia 73 kwa mwaka 2021 mpaka kufikia asilimia 93 kwa mwaka 2022.
Hayo yamebainishwa na
Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sylvester Kainda alipokuwa akiwasilisha
taarifa ya mashauri kwenye Mkutano wa Mwaka ambao umefunguliwa leo tarehe 27
Julai, 2023 na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
“Kiwango cha kumaliza
mashauri kwa kipindi cha mwezi Januari-Disemba 2022 kilikuwa ni asilimia 93.
Hivyo Mahakama ya Rufani kwa kipindi cha Januari-Disemba 2022 ilikuwa na uwezo
wa kumaliza asilimia 93 ya mashauri yanayosajiliwa. Katika kipindi cha mwaka
2021, kiwango cha kumaliza mashauri kilikuwa ni asilimia 73, hivyo kasi ya
kumaliza mashauri imepanda kwa asilimia 20,” amesema.
Mhe. Kainda ameueleza
Mkutano huo unaofanyika katika Hoteli ya Nashera mjini hapa kuwa Mahakama ya
Rufani ilianza mwaka mpya wa 2022 ikiwa na jumla ya mashauri 5,054 ambayo
yalibaki kufikia Disemba 2021. Amesema kuwa Januari - Disemba 2022, Mahakama
hiyo ilisajili jumla ya mashauri 2,040 na kati ya hayo 29, sawa na asilimia 31
ya mashauri yote ni yenye asili ya jinai na 1,411, sawa na asilimia 9 ni yenye
asili ya madai.
Msajili wa Mahakama ya
Rufani amesema kuwa mashauri yaliyosikilizwa kwa kipindi cha Januari hadi
Disemba 2022 yalikuwa 1,890 yanayojumuisha 651 ambayo ni ya jinai na mengine 1,239
ya madai.
Ameeleza kuwa katika kipindi
tajwa, jumla ya maombi 113 ya upande mmoja ya zuio la utekelezaji yalisikilizwa
na kutolewa uamuzi na kati ya hayo mashauri mawili kutoka Kanda za Shinyanga na
Tabora yalisikilizwa kwa njia ya mtandao.
“Katika kipindi cha
Januari hadi Disemba 2022, jumla ya mashauri 1,890 yalisikilizwa, ikiwa ni
ongezeko la mashauri 523 kutoka mashauri 1,367 yaliyosikilizwa mwaka 2021,”
Mhe. Kainda amesema.
Amebainisha pia kuwa hadi
Disemba 2022 kulikuwa na jumla ya mashauri 5,204 yaliyobakia na kati ya hayo,
1,990 ni ya jinai na mengine 3,214 ni yenye asili ya madai.
Akizungumzia hali ya
utoaji haki katika Mahakama hiyo ya juu hapa nchini, Mhe. Kainda amebainisha
kuwa kwa mujibu wa kalenda ya Mahakama ya Rufani, vikao 34 vilipangwa kufanyika
katika Kanda 15 ambazo ni Dar es Salaam, Mbeya, Arusha, Mwanza, Iringa, Tabora,
Mtwara, Dodoma, Shinyanga, Tanga, Musoma, Kigoma, Bukoba, Zanzibar na Moshi.
“Vikao vyote vilifanyika
kwa asilimia 100. Kipindi cha Januari-Disemba, 2022, jumla ya mashauri 2,128
yalipangwa kusikilizwa, kati ya hayo, 1,890 yalisikilizwa na kuamuliwa, sawa na
asilimia 89 ya mashauri yote. Aidha, mashauri 238 yaliahirishwa kutokana na
sababu mbalimbali,” amesema.
Amezitaja baadhi ya
sababu zilizopelekea kuahirisha kwa mashauri hayo kama wadaawa kuwasilisha nyaraka
zenye mapungufu ya kisheria na wengine kuomba kuwasilisha kumbukumbu ambazo
hazijakamilika na kutofika mahakamani kwa wadaawa siku ya shauri au
kutokupatikana.
Sababu zingine ni wadaawa
kuugua au kufariki au makampuni kufungwa, maombi ya wadaawa kuweka au
kubadilisha Mawakili, uwepo wa maombi ya kumaliza mgogoro nje ya Mahakama na
kuwepo na maombi madogo yanayosimamisha au kuchelewesha usikilizaji wa shauri
mama.
Mhe. Kainda ametaja
mafanikio kadhaa yaliyopatikana katika kipindi husika, ikiwemo kuendelea
kupungua kwa mashauri ya mlundikano kutoka mashauri 707, asilimia 14 Disemba
2021 mpaka mashauri 254, asilimia tano Disemba 2022 na kuongezeka kwa kiwango
au kasi ya kumalizika kwa mashauri (clearance rate) kutoka asilimia 73 Disemba
2021 mpaka kufikia asilimia 93 Disemba 2022.
Amesema pia kuwa
kumekuwepo na hali ya kupungua kwa mzigo wa mashauri kwa jopo (workload) kutoka
mashauri 917 kwa jopo Disemba 2021 mpaka kufikia mashauri 887 Disemba 2022, kufanya
vikao vyote kwa asilimia 100 kama ilivyopangwa katika kalenda ya Mahakama na
kuendelea kupungua kwa mashauri yanayoahirishwa kutoka 278 Disemba 2021 mpaka
kufikia mashauri 238 Disemba 2022.
Msajili wa Mahakama ya
Rufani ameeleza kuwa pamoja na hali nzuri na inayoridhisha katika kusikiliza
mashauri, bado kuna changamoto kadhaa zinazowakabili, ikiwemo kuendelea kuwepo
mashauri ya mlundikano na mzigo wa kila jopo wa mashauri 1,013 wakati uwezo ni
mashauri 297 kwa mwaka.
Ametaja changamoto
zingine kucheleweshwa kwa vitabu vya rufaa katika mashauri ya jinai, uwepo wa
mzigo mkubwa wa mashauri na upatikanaji mgumu wa wadaawa wa mashauri ya madai
na yale ya jinai, hasa kwa wahusika ambao wamemaliza vifungo au wamepata
msamaha.
Naibu Wasajili Mahakama ya Rufani (juu na chini) wakimsikiliza Msajili wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Sylvester Kainda (hayupo katika picha) alipokuwa anawasilisha taarifa yake.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni