·Naibu Waziri aifananisha na Mahakama za Kimataifa
·Asema maboresho yaliyofanyika kuongeza kasi ya utoaji haki nchini
Na Faustine Kapama-Mahakama
Naibu Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu,
Mhe. Patrobas Katambi ameupongeza uongozi wa Mahakama ya Tanzania, chini ya Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa mageuzi makubwa ambayo umefanya
kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa haki kwa wananchi.
Mhe. Katambi ametoa
pongezi hizo leo tarehe 14 Julai, 2023 alipokuwa anazungumza kwenye Mkutano wa
Saba wa Kamati ya Utatu yenye jukumu la kuweka mikakati kumaliza mashauri yote kwa
wakati yanayofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi.
Mkutano huo ambao
umefanyika kwenye Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere jijini Dar
es Salaam umefunguliwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Mustapher Mohamed Siyani.
“Kwa niaba ya Serikali, nimpongeze sana Jaji
Mkuu, wewe Jaji Kiongozi na viongozi wengine wa Mhimili wa Mahakama, kwa kweli
imani ni kubwa sana. Mimi ni shuhuda, kwa maana majukumu yale ambayo yamewekwa kimahakama
ni tofauti sana tunayoyaona kwa sasa. Hali ya sasa ipo tofauti kubwa, mmefanya
maboresho makubwa katika kuongeza kasi ya utoaji haki nchini,” amesema.
Naibu Waziri amesema
anaiona Mahakama ya Tanzania kama Mahakama za Kimataifa kwa kupiga hatua kubwa ambayo
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yatapunguza mlundikano
wa mashauri na changamoto mbalimbali.
“Mmeenda mbali zaidi
kidijitali katika usikilizaji wa mashauri. Tutaanza sasa kuziona zile za ICJ (The
International Court of Justice) na ICC (The International Criminal Court) na
kama ilivyokuwa kwenye Tribunals (Mabaraza) ya Rwanda na mengine, nadhani sasa
tunafikia kwenye hiyo hatua. Hii ni hatua kubwa sana,” amesema.
Mhe. Katambi amebainisha
pia kuwa Mahakama imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika utekelezaji wa Mpango
Mkakati, hasa kwenye kuongeza imani kwa wananchi, hivyo ushirikishaji wadau ni
jambo muhimu ili kufikia mafanikio zaidi yanayokusudiwa.
“Kila mmoja ajue malengo
mliyonayo, mipango, mikakati ambayo mnataka kufikia katika utoaji wa haki na
sisi ni sehemu yake,” amesema huku akipongeza kauli mbiu iliyowekwa katika Mkutano
huo ambayo inaweza kuchagiza ukuaji wa uchumi kwa mfumo wa usuluhishi.
Kauli mbiu ya Mkutano
huo ni “Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro ya Kazi kwa Njia ya Usuluhishi katika
Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau.”
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni