Na Faustine Kapama-Mahakama
Mahakama Kuu ya Tanzania,
Divisheni ya Kazi imetekeleza kwa ukamilifu jukumu la kikatiba la utoaji haki
kwa wananchi kwa kumaliza jumla ya mashauri takribani 2,000 yaliyopokelewa kwa
kipindi cha mwaka mmoja.
Hayo yamebainishwa na
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania katika Divisheni hiyo, Mhe. Kassian
Enock alipokuwa anawasilisha taarifa ya utekelezaji kazi katika Mahakama hiyo
kwenye Mkutano wa Saba wa Kamati ya Utatu yenye jukumu la kuweka mikakati kusaidia
kumaliza mashauri kwa wakati.
“Mashauri yaliyobaki
Julai 2022 yalikuwa 847. Mashauri yaliyosajiliwa kuanzia Julai, 2022 mpaka
Juni, 2023 ni 1,455. Mashauri yaliyoamuliwa Julai 2022 mpaka Juni, 2023
yalikuwa 1,999, sawa na asilimia 137 ya mashauri yote 1,455 yaliyopokelewa
katika kipindi hicho cha mwaka mmoja. Mashauri yaliyobaki hadi Juni, 2023
yalikuwa 303,” amesema.
Naibu Msajili amebainisha
kuwa kati ya mashauri hayo 303 yaliyobaki, ni mashauri matatu (3) tu yenye umri
wa miaka miwili (backlog) ambayo hayajaamuliwa. Amefafanua kuwa mashauri hayo
ni ya ukaziaji deni tuzo (execution) na yameshindwa kuendelea kwa sababu kuna
amri ya kusimamisha utekelezaji kusubiri maamuzi ya Mahakama ya Rufani.
Mhe. Enock aliyekuwa anawasilisha
taarifa hiyo kwa niaba ya Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Rashid Ding’ohi,
amefafanua zaidi kuwa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi katika kusikiliza mashauri
imekuwa inatumia njia mbili, yaani usikilizaji wa kawaida na ule wa vikao maalum.
Amesema kuwa kuanzia
kipindi cha mwezi Julai, 2022 hadi Juni, 2023 vimefanyika jumla ya vikao
(Session na Crash Programme) 23, ambapo Majaji wamefanya vikao 17 na Naibu
Wasajili wamefanya vikao sita (6).
“Katika vikao hivyo,
jumla ya mashauri 653 yalipangwa. Mashauri yaliyosikilizwa na kumalizika kwa
njia hiyo ya vikao ni 472. Mashauri 181 yaliyobaki yapo kwenye hatua mbalimbali
ya usikilizwaji, hukumu na uamuzi,” Mhe. Enock amesema.
Amebainisha pia kuwa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi imekuwa ikitumia mfumo wa Audio Visual Recording System na Mkutano Mtandao (Video Conferencing) katika kusikiliza mashauri yaliyoko mbele ya Majaji na kuwapunguzia waadawa gharama za kuhudhuria mahakamani hata kama wako mbali na Mahakama.
Naibu Msajili amewaambia
wajumbe wa Mkutano huo kuwa matumizi ya mfumo huo pamoja na mifumo mingine ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yamewezesha upatikanaji wa haki kwa wakati na
kutimiza matakwa ya nguzo ya pili ya Mpango Mkakati wa Mahakama.
Mpango Mkakati wa
Mahakama ya Tanzania wa Miaka Mitano (2020/21- 2024/25) umejengwa chini ya
nguzo tatu imara zinazotegemeana. Nguzo ya kwanza inahusu utawala bora,
uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali; nguzo ya pili inahusu upatikanaji wa
haki kwa wakati na nguzo ya tatu inayohusu imani kwa wananchi na ushirikishwaji
wa wadau.
Mkutano huo wa siku moja
ambao umehudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali wa Mahakama umefunguliwa na Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani ambaye amehimiza
ushirikiano baina ya Serikali, Mahakama na wadau wote katika utatuzi
wa migogoro, ikiwemo ya kazi, ili kujenga jamii yenye amani na utulivu na
kuimarisha mazingira ya kukua kwa uchumi nchini.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni