Ijumaa, 14 Julai 2023

JAJI KIONGOZI AHIMIZA SERIKALI, MAHAKAMA, WADAU KUSHIRIKIANA UTATUZI WA MIGOGORO

Na Faustine Kapama-Mahakama

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani amehimiza ushirikiano baina ya Serikali, Mahakama na wadau wote katika utatuzi wa migogoro, ikiwemo ya kazi, ili kujenga jamii yenye amani na utulivu na kuimarisha mazingira ya kukua kwa uchumi nchini.

Mhe. Siyani ametoa wito huo leo tarehe 14 Julai, 2023 alipokuwa anafungua Mkutano wa Saba wa Kamati ya Utatu katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam. Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Umuhimu wa Utatuzi wa Migogoro ya Kazi kwa Njia ya Usuluhishi katika Kukuza Uchumi Endelevu: Wajibu wa Mahakama na Wadau.”

“Jamii yoyote isiyo na mifumo thabiti ya utatuzi wa migogoro iko kwenye hatari ya kuingia kwenye machafuko. Ili kujenga jamii yenye amani na utulivu na kuimarisha mazingira ya kukua kwa uchumi wa nchi yetu, ni lazima utatuzi wa migogoro, ikiwemo ya kazi, upewe kipaumbele.

“Ili hilo litokee, ushirikiano baina ya Serikali, Mahakama na wadau wote ni jambo lisiloepukika. Kila mdau analo jukumu la kufanya katika utatuzi wa migogoro na mikutano kama hii inatupa nafasi ya kukumbushana majukumu yetu,” Jaji Kiongozi amesema.

Mhe. Siyani amesema utatuzi wa migogoro kwa usuluhishi sio tu jukumu la kikatiba bali pia njia hiyo imeonekama kuwa nyenzo inayoweza kupunguza gharama na muda wa wadaawa kuendesha mashauri yao na kudumisha maelewano mahala pa kazi, mambo ambayo hupunguza athari kwa uzalishaji na kufanya ukuaji wa uchumi kuwa endelevu.

Ni matumaini yake kuwa wadau wa Mahakama ya Kazi, kama ilivyo kwa wadau wengine wote wa Mahakama, watathamini na kushiriki kikamilifu katika jitihada zote zenye lengo la kuimarisha utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi.

Jaji Kiongozi pia amezungumzia wajibu wa Serikali, wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi na waajiri na wawakilishi binafsi katika muktadha mzima wa utatuzi wa migogoro nchini.

Amesema Serikali kama mmoja wa wadau wa haki, inao wajibu wa kuhakikisha mazingira ya uwekezaji, biashara na shughuli mbalimbali zinazozaa ajira hayazalishi migogoro na pia kutengeneza mazingira yatakayo viwezesha vyombo vya utoaji haki kutimiza wajibu wake.

Kwa upande mwingine, Jaji Kiongozi amesema wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi na wawakilishi wa waajiri, wanawajibu wa kuwasaidia wafanyakazi na waajiri kutimiza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, na hivyo kupunguza migogoro mahali pa kazi.

Kuhusu wawakilishi binafsi, Mhe. Siyani amesema ushiriki wao katika utatuzi wa migogoro ya kazi ni jambo lenye baraka za kisheria. Amesema wawakilishi binafsi walikusudiwa kuwa namna rahisi ambayo wafanyakazi wangeweza kupata uwakilishi wanapotafuta haki zao.

“Hata hivyo, ukosefu wa usimamizi katika eneo hili umezalisha malalamiko ya kimaadili dhidi ya wawakilishi binafsi. Zipo taarifa za wawakilishi binafsi kufanya kazi za kiuwakili kwa kuwatoza gharama kubwa wafanyakazi wanao wawakilisha.

“Ni vema wadau wakajadiliana na kupendekeza namna bora ya kuimarisha eneo hili ili nia ya kuruhusu wawakilishi binafsi iliyokusudiwa isitumiwe vibaya na kufanyika kikwazo kwa usuluhishi ama utatuzi wa migogoro,” amesema.

Jaji Kiongozi alizungumzia pia suala la utekelezaji wa tuzo na amri za Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) kwenye Kanda za Mahakama Kuu kote nchini, jambo ambalo limesababisha mlundikano wa mashauri ya utekelezaji.

Ameshauri wadau kujadili na kuona kama wakati umefika wa kubadilisha hali hiyo ili kupunguza mlundikano wa mashauri hayo unaochelewesha hatua ya mwisho ya upatikanaji wa haki za wadaawa.

Awali, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt Yose Mlyambina aliwaeleza wajumbe wa Mkutano huo kuwa Kamati ya Utatu inalojukumu la kuweka mikakati itakayosaidia kumaliza mashauri yote yanayofunguliwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi kwa wakati.

Amesema jukumu la Kamati linaenda sanjari na Dira ya Mahakama ya Tanzania ya kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati na katika kutimiza Dira hiyo, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi imejiwekea mikakati mbalimbali.

“Baadhi ya mikakati hiyo ni kuhakikisha kuwa mashauri yanayofunguliwa yanaisha ndani ya mwaka mmoja au pengine chini ya muda huo. Ili hayo yatimie, mkakati wetu mwingine ni kuwashirikisha wadau kwa karibu ikiwemo kutoa elimu ili tuweze kwenda kwa pamoja,” Mhe. Dkt. Mlyambina amesema.

Amebainisha pia kuwa nguzo ya tatu ya mpango mkakati wa Mahakama, inasisitiza   kuongeza imani kwa wananchi na ushilikishwaji wa wadau na katika kutekeleza nguzo hiyo, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuanzisha tovuti ya Mahakama ya Kazi.

Jaji Mfawidhi amesema tovuti hiyo inabeba maamuzi mbalimbali ya Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu yanayohusiana na sheria za kazi, matukio yanayohusiana na Mahakama ya Kazi, sheria za kazi za Tanzania, Mikataba ya Kimataifa kuhusiana na kazi na inatoa taarifa kwa umma kuhusu mashauri (cause list) na vikao vya mashauri yaliyopangwa.

“Lengo la Tuvuti hii pamoja na mambo mengine, inasaidia wadau kupata kwa urahisi maamuzi mbalimbali, sheria na taarifa kuhusu mashauri yao,” amesema na kuongeza kuwa Divisheni ya Kazi pia imeunda kamati ya elimu kwa ajili ya kutoa elimu kwa watumishi na wadau kuhusiana na masuala ya kazi na taratibu zinazotakiwa kuzingatiwa katika ufunguaji wa mashauri.

Mkutano huo umehudhuriwa na wadau na viongozi mbalimbali wa Serikali na Mahakama, wakiwemo Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Mhe. Patrobas Katambi, Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na Arusha. Majaji wengine wa Mahakama Kuu ya Tanzania, viongozi mbalimbali wanaohusiana na masuala ya kazi na wadau wengine pamoja na watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Mohamed Siyani (juu na chini) akisisitiza jambo alipokuwa anafungua Mkutano wa Saba wa Kamati ya Utatu katika Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam leo tarehe 14 Julai, 2023.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt Yose Mlyambina akieleza jambo alipokuwa anatoa neno fupi la kumkaribisha Jaji Kiongozi kufungua mkutano huo.
Sehemu ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa kwenye mkutano huo. 
Sehemu ya wajumbe na wadau mbalimbali (juu na chini) wakifuatilia yaliyokuwa yanajiri kwenye mkutano huo ambao umefunguliwa na Jaji Kiongozi. 

Sehemu ya watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Divisheni ya Kazi (juu na chini) wakiwa kwenye mkutano huo. 

Mkutano unaendelea. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni