Alhamisi, 13 Julai 2023

JAJI LATIFA MANSOOR AWA MWENYEKITI WA JMAT TAWI LA MASJALA KUU

  

 

 Na Magreth Kinabo - Mahakama 

 

Aliyekuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga, Mhe. Latifa Mansoor amechaguliwa kuwa   Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) tawi la Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, lilipo jijini Dar es Salaam.

 

Mhe.  Jaji Latifa amechaguliwa kushika wadhifa huo leo tarehe 13 Julai, 2023 katika uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa Kituo cha Habari cha Mahakama ya Tanzania kilichopo katika Mahakama ya Kuu Tanzania.

 

Jaji Latifa amechukua nafasi ya Mwenyekiti wa zamani  wa tawi hilo na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Katarina Mteule ambaye hivi sasa ameteuliwa kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga. 

 

Akizungumza mara baada ya kuchaguliwa, Jaji Latifa amesema anawashukuru wanachama wa tawi hilo kwa kumchagua na kuahidi kwamba atajitahidi kutimiza majukumu yake ipasavyo ili kuhakikisha tawi hilo linakuwa la mfano wa kuigwa.

 

Awali akifungua mkutano wa uchaguzi huo, Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Wilfred Dyansobera, ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu, aliwaasa wanachama wa tawi hilo kufanya kazi kwa kujituma na kuzingatia maadili, weledi, uwajibikaji, kujiepusha na matendo mabaya kama vile rushwa, ikiwemo kuwajali wateja na kuhakikisha wanapata haki zao kswa wakati.

 

“Nina washauri kutoa ushauri wenye tija katika maboresho ya miundombinu na utendaji kazi. Pia mwuishauri JMAT Taifa kwa lengo la kuleta mahusiano mazuri kati ya mwajiri na chama ili matunda yanayotarajiwa yaweze kupatikana,” amesema Kaimu Jaji Kiongozi huyo.

 

Wakati huohuo Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo akitoa mada juu ya matumizi ya mitandao ya kijamii na maadili ya Afisa wa Mahakama kwa wanachama wa tawi hilo, ambapo  amesema ni vema wakawa makini na matumizi hayo ili kuepusha migongano katika utendaji  wao wa kazi.

 

“Suala la matumizi ya mitandao ya kijamii ni jambo ambalo halikwepeki, hivyo tunapaswa kuwa waangalifu na taarifa tunayoitoa kwa jamii na kuchukua tahadhari,” amesema   Jaji Dkt. Modesta.

 

Jaji Modesta aliongeza kuwa wanachama wa tawi hilo, wanatakiwa kuwa makini na makundi ya mitandao ya kijamii wanayoingizwa.

  

Katika hatua nyingine Meneja Mahusiano wa Mikopo ya Nyumba kutoka Benki ya NMB, Bi. Pauline Sangali    aliwaelimisha wanachama wa tawi hilo kuhusu bima ya akiba na afya salama zitolewazo na benki hiyo. 

 

Mkutano huo ulihudhuriwa na Majaji Wafawidhi, Majaji, Naibu Wasajili, Mahakimu na viongozi wa JMAT.

 Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) tawi la Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu lilipo jijini Dar es Salaam, Mhe. Jaji Latifa Mansoor (kushoto) akizungumza jambo mara baada ya kuchaguliwa. (Katikati) ni Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Wilfred Dyansobera, ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu na (kulia) ni Katibu wa mkutano huo, Mhe. Simon Laizer.

 Kaimu Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Wilfred Dyansobera, ambaye ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu akitoa hotuba katika mkutano huo wa JMAT.

 Mwenyekiti wa zamani  wa tawi hilo na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Katarina Mteule ambaye hivi sasa ameteuliwa kuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga akitoa neno la shukurani. 

Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Dkt. Modesta Opiyo akitoa mada juu ya  matumizi way a mitandao ya kijamii na maadili ya Afisa wa Mahakama  kwa wanachama wa tawi hilo.


Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Tanzania (JMAT) tawi la Mahakama Kuu ya Tanzania Masjala Kuu lilipo jijini Dar es Salaam, Mhe. Jaji Latifa Mansoor (waliokaa wav pili kushoto) akiwa katika picha ya Pamoja na wanachama wa JMAT wa tawi hilo.


picha juu na chini ni baadhi ya wanachama wa tawi hilo wakiwa katika mkutano huo. 

Meneja Mahusiano wa Mikopo ya Nyumba kutoka Benki ya NMB, Bi. Pauline Sangali   akitoa  elimu kuhusu bima ya akiba na afya salama zitolewazo na benki hiyo.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni