Na Stephen Kapiga-Mahakama, Mwanza
Jaji
wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania, Mhe. Stella Mugasha amewataka Mahakimu kusoma
sheria kwa makini wanapotekeleza majukumu yao ya utoaji haki kwa wananchi,
ikiwemo kusikiliza mashauri na kutoa maamuzi.
Mhe.
Mugasha ametoa wito huo jana tarehe 12 Julai, 2023 alipokuwa anazungumza na Mahakimu
wa Mahakama zilizopo Mwanza Mjini wakati wakijadili changamoto mbalimbali
wanazokutananazo wakati wa uendashaji wa mashauri.
Majadiliano
hayo yalifanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo kwenye Kituo Jumuishi cha Utoaji
Haki (IJC) Mwanza.
“Nawasihi
sana msiogope kuzisoma sheria zote kwa umakini mnapofanya maamuzi katika
mashauri mnayoendesha, kwani mliapa kufanya kazi kwa kufuata sheria pasipo huba
wala upendeleo. Mkiwa kama kisima kikubwa cha Majaji wajao muwe na kawaida ya
kusoma sheria na kuitafsiri ipasavyo,” alisema.
Naye
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. Chiganga
Tengwa aliongelea maeneo yenye utata ambayo Mahakimu wamekuwa wakikutananayo wakati
wa kufanya maamuzi.
Alitoa
mfano pale panapokuwa na mgongano wa sheria mbalimbali, hivyo kupelekea upande
mmoja kuonekana kama hautendewi haki.
“Ukisoma
kifungu cha 25 cha Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Na. 1 ya 2020 na pia ukisoma
kifungu cha 97 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (mamlaka ya mijini) utaona kuna
huo mgongano juu ya nani anapaswa kuwa served na muda wa notice hiyo,” alisema.
Majadiliano
hayo yalilenga kuwajengea uelewa Mahakimu hao namna bora ya kufikia maamuzi
katika mashauri wanayoendesha, hatua itakayowawezesha kufanya kazi kwa
kujiamini na usahihi, hivyo kuongeza Imani ya jamii kwa Mahakama.
Maeneo waliyogusia katika majadiliano hayo yalihusu namna ya kuchukua ushahidi kwa mtu mwenye matatizo ya akili, namna ya kufanya utekelezaji wa tuzo mbalimbali za Mahakama, kushughulikia mashauri ya mirathi na yale yanayoihusisha Serikali kwa kuzingatia Sheria za Serikali za Mitaa na Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Na.1 ya mwaka 2020.
Naibu Msajili Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Mwanza, Mhe. Chiganga Tengwa akieleza jambo wakati wa majadiano hayo.
Baadhi ya Mahakimu (juu na picha mbili chini) walioshiriki katika majadiliano hayo yaliyofanyika jana tarehe 12 Julai, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Kituo Jumuishi cha Utoaji Haki Mwanza.
(Habari hii imehaririwa na FAUSTINE KAPAMA-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni